Na Mwandishi Maalum, Dodoma
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi amejiandikisha kwenye daftari la wakazi katika mtaa wake, eneo la Kilimani, jijini Dodoma leo tarehe 18, Oktoba 2024.
Akizungumza baada ya kujiandikisha, Balozi Nchimbi aliwasisitiza wananchi umuhimu wa kujitokeza kwa wingi kuandikishwa, akisema kuwa ni hatua muhimu katika kuhakikisha ushiriki wao kwenye mchakato wa kidemokrasia.
Uandikishaji wa wapiga kura wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, kwenye daftari la wakaazi, ulianza tarehe 11 Oktoba, 2024 na utamalizika tarehe 20 Oktoba 2024.
Balozi Nchimbi amewahimiza wananchi kutumia siku zilizobaki kutimiza haki yao ya kikatiba ya kuchagua viongozi bora wa Serikali za Mitaa mwezi ujao, akisisitiza kuwa kila kura inahesabika na inaweza kuleta mabadiliko makubwa kwenye jamii, ikizingatiwa kuwa viongozi watakaochaguliwa watakuwa na jukumu la kusimamia maendeleo ya mitaa yao.
Balozi Nchimbi amesisitiza umuhimu makundi yote katika jamii kushiriki kikamilifu, hususan vijana na wanawake, kutambua nafasi yao ya kipekee katika mchakato huu, ikiwa pia ni sehemu muhimu kwao kujihusisha na siasa kwa lengo la kuleta maendeleo katika kijamii.
Pamoja na kuwasisitiza wananchi wajiandikishe na kujitokeza kupiga kura siku ya uchaguzi, Balozi Nchimbi alisema uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni fursa kwa wananchi kuchagua viongozi wenye maono na uwezo wa kuongoza na kusimamia shughuli za maendeleo kama vile elimu, afya, maji safi, na miundombinu.
Aidha, Katibu Mkuu ameendelea kuwataka wananchi na wadau wote wa uchaguzi, kudumisha amani na mshikamano, kuepuka kuchochea chuki katika jamii, na kuzingatia taratibu za kisheria, ili kuhakikisha maslahi ya taifa na tija kwa wananchi, vinakuwa mbele, kabla, wakati, na baada ya uchaguzi.
0 Comments