Ticker

6/recent/ticker-posts

WANAOKUSANYA BETRI CHAKAVU BILA KUFUATA TARATIBU, AGENDA WATOA NENO KWA WADAU

Na Said Mwishehe, Michuzi TV

BARAZA la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira(NEMC)limewashauri watu wote wanaojihusisha na kukusanya betri chakavu na Kwenda kuuza katika viwanda vinavyochakata betri hizo kuhakikisha wanazingatia kanuni, taratibu na maelekezo yaliyopo kwenye vibali.

Lengo ni kuhakikisha wanaojihusisha na biashara hiyo kuifanya katika mazingira yaliyosalama ili kuepuka madhara ya kiafya na kimazingira katika jamii.

Ushauri huo umetolewa leo Oktoba 22,2024 jijini Dar es Salaam na Meneja wa Uzingatiaji kutoka NEMC Hamad Taimuru aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu katika semina iliyoandaliwa na Asasi ya AGENDA kwa kushirikana na baraza hilo pamoja na Taasisi ya Utafiti ya Oeko-Institut ya Ujeruman kwa ufadhili wa Shirika la Ushirikiano wa kimataifa la Ujeruman(GIZ).

“Kwa jamii tunaisa iache kumwaga asidi kwenye mazingira, wakusanye mabetri na kupeleka katika viwanda ambavyo vimepewa vibali kwa ajili ya kuchakata na kujua asidi zinakwenda wapi na plastiki zinakwenda wapi.

“Mkusanyaji anachotakiwa ni kukusanya tu na kisha akauze viwandani lakini sio kumwaga maji ya asidi.Hii ni biashara japokuwa ni takataka, hivyo wafanye biashara kwa mujibu wa kanuni, taratibu na maelekezo waliyopewa wakati wanapewa vibali…

“Na wale wanaofanya kiujanja ujanja bila vibali tunawaambia ofisi zetu ziko wazi kanda zote, waje kupata vibali kwani mchakato wa kupata vibali ni rahisi, wasifanye kazi kiujanja ujanja ili.Kwa pamoja tulinde mazingira ili kuepuaka madhara ya kiafya na kinadamu.”

Akifafanua zaidi amesema kupitia semina hiyo wamebaini kuwa kuna baadhi ya viwanda wamekuwa wakipokea betri chakavu ambazo hazina asidi, hivyo ni lazima sasa kuangalia aside hiyo inakwenda wapi huko mtaani.

“Tulidhani betri zinakwenda vile vile kama zilivyo lakini tumepata taarifa betri zinapokelewa hazina maji ya asidi, hivyo lazima tujiulize zinakwenda wapi, mtu anapokea betri tani 50 lakini anakuta karibia tano tano hazina asidi.

“Hivyo lazima tufanyie kazi ili biashara iende vizuri lakini na mazingira yalindwe, tueambiwa madhara yanayoweza kutokea kutokana na kumwagika hovyo kwa asidi.”

Kuhusu semina hiyo ya wadau ambao wamekutana kuangalia namna ya kuboresha urejelezwaji wa betri chakavu nchini Tanzania, amesema wamekutana ili kujadiliana kwa pamoja na kukumbushana taratibu za usimamizi wa taka hatarishi.

“Tumeona wenzetu katika nchi nyingine wanafanyaje na sisi tunafanyaje.Tutatoka na taarifa ya pamoja ambayo itakwenda kwa wenzetu wa viwandani ambao wao wataifikisha taarifa hiyo kwa wakusanyaji wadogo kule mtaani.”

Kwa upande wake Silvani Mng’anya ambaye ni Ofisa Programu Mkuu wa AGENDA amesema katika warsha hiyo pia wamealika wadau kutoka katika manispaa hasa wanaohusika na ukaguzi na watendaji wa shughuli za urejelezwaji wa betri chakavu katika viwanda.

“Mbali ya wadau pia tumealika viwanda vinne ambavyo vimehudhuria warsha hii na tumefanya mafunzo pia kuhusu utaratibu mzuri wa uendeshaji wa shughuli hizi za uchakataji na urejelezwaji wa bertri kwa nia ya kusaidia na wale wakaguzi namna ya kuboresha utendaji wa kila siku.Kupitia warsha hii tumebaini uwepo wa mapengo lakini mafunzi hayo yatasaidia kuboresha pande zote mbili kwa maana ya wenye viwanda na wakaguzi.”

Ameongeza ujumbe mkubwa katika warsha hiyo ni ni kupunguza madhara ya madini ya risasi katika mazingira na afya kwa ujumla huku akifafanua kuwa ulifanyika utafiti miaka sita kufahamu utaratibu katika viwanda ukoje lakini umefika wakati wa kufanya tafiti itakayokuja na majibu sahihi yatakayowezesha wadau kutambua maeneo gani yanahitaji mkazo zaidi.

“Kwa kushirikiana na wadau wakiwemo wenzetu wa NEMC inaweza kutusaidia kupata takwimu halisi hasa ya kiwango cha uwepo wa betri chakavu katika maeno tunayoshi.”

Post a Comment

0 Comments