Ticker

6/recent/ticker-posts

NGUGI WA THIONGO AFARIKI DUNIA


Mwandishi maarufu na msomi mashuhuri wa fasihi ya Kiafrika, Profesa Ngũgĩ wa Thiong’o, amefariki dunia Jumatano tarehe 28 Mei 2025 akiwa na umri wa miaka 87.

Kifo chake kimethibitishwa na familia yake kupitia ujumbe wa binti yake, Wanjiku wa Ngũgĩ, aliyeandika katika ukurasa wake wa Facebook:“Ni kwa huzuni kubwa tunatangaza kifo cha baba yetu, Ngũgĩ wa Thiong’o, kilichotokea asubuhi ya leo, 28 Mei 2025. Aliishi maisha kamili, alipigana vita vyema. Kama alivyoomba kabla ya kifo chake, tusherehekee maisha na kazi zake”

Familia imesema kuwa msemaji wao, Nducu wa Ngũgĩ, atatoa maelezo zaidi kuhusu taratibu za kuadhimisha maisha yake.

Ngũgĩ alizaliwa tarehe 5 Januari 1938 katika kijiji cha Kamiriithu, karibu na Limuru, Kaunti ya Kiambu, nchini Kenya. Alijulikana kwa kazi zake bunifu, fikra za kisiasa, na msimamo wake thabiti kuhusu ukombozi wa kiutamaduni na kiakili wa Mwafrika.

Alianza kuandika riwaya kwa Kiingereza akiwa mmoja wa waandishi wa kwanza wa Kiafrika kuchapisha kazi katika lugha hiyo, akitoa kazi kama Weep Not, Child (1964), The River Between (1965), na A Grain of Wheat (1967). Hata hivyo, baadaye aligeukia kuandika kwa lugha ya mama yake – Kikuyu – kama njia ya kupinga ukoloni wa fikra na kupigania uhuru wa kweli wa Kiafrika.

Moja ya matukio muhimu katika maisha yake ni tamthilia Ngaahika Ndeenda (1977), aliyoandika kwa kushirikiana na Ngũgĩ wa Mirii, iliyomkosoa vikali mfumodume wa utawala na kusababisha yeye kufungwa bila kufikishwa mahakamani kwa karibu mwaka mmoja.

Tamthilia hii iliandikwa awali kwa lugha ya Kikuyu mnamo mwaka 1977, kwa jina la "Ngaahika Ndeenda" (I Will Marry When I Want), na baadaye ikatafsiriwa kwa Kiingereza.

Ni kazi ya kifasihi inayoshughulikia masuala ya ukoloni mamboleo, ukandamizaji wa kijamii, na mapambano ya wananchi wa kawaida dhidi ya ukandamizaji wa kisiasa na kiuchumi nchini Kenya.

Akiwa gerezani, aliandika riwaya ya Devil on the Cross kwa kutumia karatasi za chooni, kazi ambayo baadaye ilitambuliwa kama ya kipekee katika historia ya fasihi ya Kiafrika.

Baada ya kuachiwa huru, alihamia uhamishoni na hatimaye kuishi Marekani, ambako alihudumu kama Profesa mashuhuri wa Fasihi na Lugha Linganishi katika Chuo Kikuu cha California, Irvine. Katika kazi zake za kitaaluma, Ngũgĩ aliendelea kushughulikia masuala ya lugha, utambulisho, na ukombozi wa fikra.

Kitabu chake maarufu Decolonising the Mind (1986) kilikuwa mchango mkubwa katika kuelewa jinsi lugha hutumika kama chombo cha kuendeleza ukoloni wa kimawazo hata baada ya uhuru wa kisiasa. Katika maisha yake yote, alisisitiza kwamba huwezi kuikomboa Afrika kwa kutumia lugha za kikoloni pekee, bali kwa kurudi katika lugha na tamaduni za Kiafrika.

Kazi yake ya mwisho iliyochapishwa kabla ya kifo ilikuwa Decolonizing Language and Other Revolutionary Ideas (2025), mkusanyiko wa insha na mashairi uliokusanya fikra zake za takribani miongo miwili kuhusu lugha, elimu, na viongozi mashuhuri kama Nelson Mandela na Chinua Achebe.

Pia, riwaya yake ya kishairi Kenda Muiyuru (The Perfect Nine), iliyochapishwa mwaka 2020 kwa lugha ya Kikuyu, iliingia kwenye orodha ya tuzo ya kimataifa ya International Booker Prize mwaka 2021, ikiashiria upekee na uzito wa kazi zake hata katika jukwaa la kimataifa.

Katika maisha yake, Ngũgĩ aliwahi kufundisha katika vyuo vikuu mbalimbali duniani, vikiwemo Makerere (Uganda), Leeds (Uingereza), Yale, na New York University (Marekani). Alichangia pakubwa katika kulea vizazi vipya vya wasomi na waandishi.

Ngũgĩ ameacha watoto na wajukuu ambao wengi wao wameendeleza urithi wake kama waandishi, wanaharakati, na wasomi.
Baadhi ya Vitabu Vilivyoandikwa na Ngũgĩ wa Thiong’o:Weep Not, Child (1964) – Riwaya ya kwanza kuandikwa na Mkenya kwa Kiingereza.
👉The River Between (1965) – Inachunguza migongano ya mila na dini ya Kikristo.
👉A Grain of Wheat (1967) – Kuhusu mapambano ya ukombozi wa Kenya.
👉Petals of Blood (1977) – Inakosoa ubepari na unyonyaji baada ya uhuru.
👉Devil on the Cross (1980) – Iliandikwa gerezani kwa Kikuyu.
👉Matigari (1987) – Riwaya ya kishairi yenye maudhui ya kifalsafa.
👉Decolonising the Mind (1986) – Maelezo ya kina kuhusu ukoloni wa fikra.
👉Moving the Centre (1993) – Kuhusu demokrasia ya kiutamaduni.
👉Something Torn and New: An African Renaissance (2009)
👉Dreams in a Time of War (2010) – Wasifu wa maisha yake ya utotoni.
👉In the House of the Interpreter (2012) – Maisha yake ya shule.
👉Birth of a Dream Weaver (2016) – Sehemu ya tatu ya wasifu wake.
👉The Perfect Nine (2020) – Hadithi ya kihistoria kuhusu jamii ya Wakikuyu
👉The Language of Languages – Kuhusu umuhimu wa lugha za Kiafrika
👉Decolonizing Language and Other Revolutionary Ideas (2025) – Insha na mashairi kuhusu fikra za ukombozi wa kiakili.
Urithi wa Milele

Kifo cha Profesa Ngũgĩ wa Thiong’o ni pigo kubwa kwa bara la Afrika na ulimwengu wa fasihi kwa ujumla. Ameacha urithi mkubwa wa maandiko, mawazo, na mapambano ambayo yataendelea kuhamasisha vizazi vijavyo. Hakuwa tu mwandishi – alikuwa mpiganiaji jasiri wa fikra huru, lugha za Kiafrika, na hadhi ya Mwafrika.

Pumzika kwa amani, Ngũgĩ wa Thiong’o. Mchango wako hautasahaulika. 🕊️

Taarifa Imeandaliwa na MALUNDE 1 BLOG

Post a Comment

0 Comments