Kampuni ya Lake Energy Tanzania imeiomba Serikali kuchukua hatua kudhibiti uingizwaji holela wa nondo kutoka mataifa ya nje, ikieleza kuwa bidhaa hizo huuzwa kwa bei ya chini kupita kiasi, hali inayosababisha kampuni za ndani kushindwa kushindana kibiashara na hivyo kuathiri soko la ndani.
Wito huo umetolewa leo na Bw. Ally Swaleh Mbarak, Afisa Masoko wa bidhaa za viwandani kutoka Lake Energy, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara ya Sabasaba, yanayoendelea jijini Dar es Salaam. Alieleza kuwa, kuendelea kwa uingizwaji huo wa nondo kunadhoofisha ushindani wa haki na kuathiri ukuaji wa viwanda vya ndani.
Kwa upande wake, Bw. Ally Mngazija, Afisa Mauzo wa bidhaa za vilainishi vya magari kutoka kampuni hiyo, amesema Lake Energy imelazimika kubadili muundo wa vifungashio vya bidhaa zake ili kukabiliana na tatizo la uchakachuaji. Hatua hiyo inalenga kuhakikisha kuwa wateja wao wanapata bidhaa halisi na bora zinazotoka moja kwa moja kutoka kwao.
Katika kuunga mkono maonesho ya Sabasaba, Bw. Edwin Christopher, Afisa Masoko wa kampuni hiyo, ametangaza ofa maalum kwa kipindi chote cha maonesho hayo ambapo mitungi ya gesi ya ukubwa mdogo inauzwa kwa Shilingi 35,000, huku mtungi mkubwa pamoja na jiko la mafiga mawili ukiuzwa kwa Shilingi 150,000.
Bw. Christopher ameongeza kuwa Lake Energy kwa kushirikiana na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), tayari wamesambaza zaidi ya mitungi 150,000 ya gesi katika mikoa mbalimbali nchini ikiwemo Arusha, Manyara na Dodoma, kupitia zaidi ya vituo 150 vya usambazaji vya kampuni hiyo vilivyopo nchi nzima.
Lake Energy ni kampuni ya kizalendo inayojishughulisha na uzalishaji na usambazaji wa bidhaa mbalimbali za viwandani, mitungi ya gesi, mafuta, vipuri vya magari, nondo na bidhaa nyingine muhimu kwa maendeleo ya uchumi wa viwanda nchini.



0 Comments