Ticker

6/recent/ticker-posts

RC TANGA ATOA MAELEKEZO MRADI UJENZI WA BWAWA LA UMWAGILIAJI MKOMAZI






Na Oscar Assenga, KOROGWE.

MKUU wa Mkoa wa Tanga Balozi,Dkt Batilda Burian amemtaka Mkandarasi anayesimamia mradi wa Ujenzi wa Bwawa la Umwagiliaji la Mkomazi wilayani Korogwe unao gharimu kiasi cha Bilioni 18.6 kuongeza nguvu kazi ya kutosha ikiwemo kufanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati uliopangwa.

Bwawa la Umwagiliaji la Mkomazi linajengwa katika Kijiji cha Manga Mtindilo wilayani ya Korogwe ambalo linatarajiwa kuwa mkombozi mkubwa kwa Kilimo cha Umwagiliaji mkoani Tanga na mradi huo unatekelezwa na Mkandarasi China Sichuan International Cooperation Co.LTD.

Maelekezo ya Mkuu huyo wa Mkoa aliyatoa wakati alipofanya ziara ya kutembelea mradi huo akiwa na kamati ya ulinzi na usalama kwa lengo la kujionea hali ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Bwawa hilo kuhakikisha mradi huo wa kimkakati unatekelezwa kwa viwango na kwa kasi inayostahili.

Hatua hiyo ilitokana na kutokuridhishwa na kasi ya ujenzi wa mradi wa bwawa hilo kutokana na namna unavyotekelezwa hasa kwa kazi ambazo zingepaswa kutekelezwa kwa haraka zaidi .

Aidha alisema kwamba wamekuja kutembelea Bwawa hili ambalo ni muhimu kutokana na kwamba mkoa wa Tanga unatarajiakuwa kitovu cha uzalishaji wa chakula kwa mikoa ya Kilimanjaro,Manyara na Arusha kupitia mradi huo mkubwa pindi utakapokamilika

Mkuu huyo wa mkoa alimshukuru Rais Dkt Samia Suluhu kwa maono yake na kuamua kutenga zaidi ya Bilioni 18.2 kwa ajili ya mradi huo mkubwa na kuongeza tena Milioni 400 hivyo kufikia Bilioni 18.6 ikiwa ni dhamira ya kweli kuhakikisha kilimo cha umwagliaji kinakuwa nguvu ya usalama wa chakula.

Alisema kwamba mradi huo ni muhimu kutokana na kwamba mabadiliko ya tabia ya nchi mvua ambazo zilitarajiwa kunyesha mkoa wa Tanga hazikunyesha kwa wakati wala kwa kiwango kilichokusudiwa hivyo hiyo ni ishara kwamba hawawezi kutegemea kilimo cha mvua pekee ndio maana wanasisitiza kilimo cha uhakika ni cha umwagiliaji.

Awali akizungumza Mhandisi kutoka kwa Mkandarasi Andrew Magungu alisema kwamba wamepokea maelekezo ya kiongozi huyo na kuhaidi kuyafanyia kazi ili kuhakikisha malengo ya mradi huo yaliyowekwa ya kukamilisha mradi huo kwa wakati.
Naye kwa upande wake Meneja wa Mradi huo ,Mhandisi Leonard Someke maendeleo ya kazi mpaka sasa ipo asilimia 84.9 na mradi huo utakapokamilika unatarajiwa kuwanufaisha zaidi ya wananchi 20,000 kutoka Kata saba ambapo ni jumla ya vijiji 28 kutoka wilaya ya Korogwe kwa kuwawezesha kulima mara mbili hadi tatu kwa mwaka tofauti na awali .


Eneo ambalo litakapomwagiliwa litakuwa ni Hekta 9000 sawa na Ekari 22,500 huku faida za mradi huo zikielezw kupunguza athari ya mafuriko yanayokumba mashamba ya wakulima .

Post a Comment

0 Comments