Benki ya Biashara Tanzania (TCB) imezindua Kampeni Kabambe ya Msimu wa Sikukuu yenye lengo la kuwazawadia wateja wanaotumia kadi ya Popote Visa kufanya malipo, ambapo wateja watapata rejesho la asilimia 10 kwa kila muamala utakaokidhi vigezo vilivyowekwa na benki.
Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi wa Masoko na Uhusiano wa Umma wa TCB, Bw. Alex Dwashi, alisema kampeni hiyo inaonyesha dhamira ya benki kuimarisha ujumuishi wa kifedha pamoja na kuhamasisha matumizi ya malipo ya kidijitali, hasa katika kipindi cha sikukuu ambacho hutajwa kuongeza matumizi ya kifedha miongoni mwa wananchi.
Kwa upande wake, Afisa Mkuu wa Huduma za Kidijitali na Ubunifu wa TCB, Jesse Jackson, alisema rejesho hilo la asilimia 10 limeandaliwa mahsusi kuongeza hamasa ya matumizi ya mifumo ya malipo isiyotegemea fedha taslimu ambayo ni salama, rahisi na ya kisasa. Aliongeza kuwa TCB inaendelea kuwekeza katika teknolojia ili kuboresha huduma na kuongeza ufikikaji wa huduma za kifedha kwa wateja.
Naye, Mkurugenzi wa Biashara za Wateja Wadogo na wa Kati wa TCB, Lilian Mtali, alisema kampeni hiyo itaimarisha utoaji huduma kwa wateja na kuendeleza maboresho ya kimkakati ndani ya benki, sambamba na kusukuma mbele ajenda ya kidijitali katika sekta ya fedha.
Kampeni hii itadumu katika msimu mzima wa sikukuu, na TCB imewataka wateja wake kuhuisha na kutumia kadi zao za Popote Visa ili kunufaika na ofa hiyo. Benki imesisitiza kuwa kadi hiyo inakubalika duniani kote na hutoa taarifa za miamala papo hapo, hivyo kuwa njia salama na rahisi ya kufanya malipo ndani na nje ya nchi.







0 Comments