-Zaidi ya Kaya 5,600 kunufaika
Wananchi wa vitongoji vya Msokole na Funguni Kijiji cha Mnazi Kata ya Nalingu Mkoani Mtwara wameishukuru Serikali kwa kuwapelekea mradi wa Umeme unaotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ambao wamesema unakwenda kubadili maisha yao.
Wametoa shukrani hizo kwa nyakati tofauti Januari 28, 2026 wakati wa kumtambulisha Mkandarasi atakayetekeleza mradi wa Kusambaza Umeme mkoani humo Kampuni ya DIEYNEM Co Ltd.
“Tunaishukuru Serikali, hatimaye nasi tumefikiwa na mradi ambao utaimarisha shughuli zetu za uvuvi, umeme utatuwezesha kuhifadhi mazao ya uvuvi tofauti na ilivyo sasa kwani inatulazimu kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hii,” amesema Issa Mohamed Mkazi wa Kitongoji cha Msokole.
Mjasiriamali Kitongoji cha Funguni, Himid Ramadhan amesema kuwa umeme ni fursa na kwamba kufika kwa mradi kutamuwezesha kupanua biashara yake na kuanza kuuza vinywaji baridi lakini pia vijana wengine kitongojini hapo wataweza kubuni miradi ya kuwaongezea vipato ikiwemo biashara ya saluni.
Kwa upande wake Fadhila Hassan Mkazi wa Kitongoji cha Msokole amesema umeme unakwenda kuwakwamua kimaisha kwani kwa sasa biashara na shughuli nyingi za kijamii zinahitaji umeme na ameipongeza Serikali kwa mradi.
Awali akimtambulisha Mkandarasi kwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala, Meneja Usimamizi wa Miradi ya Kusambaza Umeme wa REA, Mhandisi Deogratius Nagu alisema REA inatekeleza mradi wa shilingi bilioni 15,369,843,407.29 wa kusambaza umeme katika vitongoji 175 utakaonufaisha kaya 5,646 mkoani humo.
Pia Mha. Nagu alisema mradi utatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu na ameiomba Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kushirikiana na REA kufikisha elimu na taarifa sahihi kwa wananchi, ushirikiano kwenye ulinzi na usalama wa vifaa vya Mradi sambamba na kuhamasisha wananchi kuunganishiwa umeme hasa ikizingatiwa kuwa umeme ni fursa ya kiuchumi na kijamii.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Mhe.Kanali Patrick Sawala alimemsisitiza Mkandarasi kuhakikisha anafanya kazi kwa kuwashirikisha viongozi katika ngazi mbalimbali ili kuepuka changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji wa mradi.
“REA mnatekeleza maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa vitendo, ninawapongeza kwa hili ila ninawasisitiza mnapofika kwenye maeneo ya miradi jitambulisheni viongozi na wananchi wa maeneo husika wawatambue na mtafanikiwa kuepuka migogoro isiyo ya lazima na pia ulinzi na usalama utakuwa mikononi mwao kwakuwa mmewashirikisha,” amesisitiza Mkuu wa Mkoa Kanali Sawala.
Naye Meneja Miradi wa Mkandarasi, Mha. Novatus Lyimo amemuhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa mradi utatekelezwa kwa ufanisi na utakamilika kwa wakati na kwamba watafanya kazi kwa ukaribu na wananchi na kwamba watatoa ajira zisizo za kitaalam kwa wananchi wa maeneo ya mradi.









0 Comments