Katika kuenzi siku ya kuzaliwa Rais, wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji (OR-MU), Mhe. Dkt. Pius Chaya, ameshiriki zoezi la upandaji miti katika Makao Makuu ya Ofisi hiyo, Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma.
Zoezi hilo ambalo limefanyika leo tarehe 27 Januari 2026 linaungana na jitihada za kitaifa zinazoendelea kufanyika katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kuongeza uoto wa asili na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
“Natoa wito kwa wengine kuunga mkono juhudi za Mhe. Rais kwa kupanda miti ya kutosha katika mazingira yetu”. Amesema Dkt. Chaya.
Dkt. Chaya ameongeza kuwa, nchi zetu zinaathiliwa sana na matatizo ya ukame, na kukosekana kwa mvua, hivyo kupitia kampeni ya Mhe. Rais ya kuhamasisha upandaji miti ni hatua nzuri ambayo itaenda kuzitatua changamoto hizo.
Aidha, Mhe. Naibu Waziri, aliwaongoza wafanyakazi wa Ofisi hiyo kukata keki ikiwa ni Ishara ya kuadhimisha siku ya kuzaliwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, wakithamini na kutambua mchango wake katika kuleta maendeleo ya Taifa.
Sambamba na hilo, Mhe. Naibu Waziri alitumia fursa hiyo, kukagua jengo la Wizara linaloendelea kujengwa katika Mji wa Serikali Mtumba ambapo ujenzi wake umefikia asilimia zaidi ya 80 ya utekelezaji, Mhe. Dkt. Chaya amemwelekeza Mkandarasi kukamilisha na kukabidhi jengo hilo kwa mujibu wa mkataba.





0 Comments