Na Mwandishi Wetu
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limewahakikishia wananchi kuwa bidhaa za pombe zinazozalishwa nchini na zinazoingizwa kutoka nje ni salama kwa matumizi, huku likionya dhidi ya madhara makubwa yanayotokana na matumizi holela ya pombe katika jamii.
Akizungumza wakati akitoa elimu kwa wananchi wa Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, Kaimu Meneja wa Tathmini ya Hatari katika Chakula TBS, Bi. Immaculatha Tarimo, amesema TBS ina wajibu wa kuhakikisha usalama na ubora wa bidhaa zote za chakula, ikiwemo pombe, pamoja na kutoa elimu kuhusu vihatarishi vya usalama wa chakula na namna ya kuviepuka.
Ameeleza kuwa vihatarishi vya chakula vinaweza kuwa vya kikemikali, kibaiolojia au vitu halisi kama vile mchanga, chuma, nywele na takataka, ambavyo vinaweza kuingia katika chakula wakati wowote ndani ya mnyororo wa thamani wa uzalishaji hadi matumizi.
“Kama mdhibiti wa viwango, TBS hutoa leseni za ubora kwa viwanda, husajili bidhaa za pombe, hufanya ukaguzi sokoni na uchunguzi wa kimaabara ili kuhakikisha bidhaa zinazomfikia mlaji ni salama,” amesema Tarimo.
Kuhusu malalamiko ya hivi karibuni kutoka kwa jamii yanayohusisha madhara ya kiafya baada ya unywaji wa pombe, Tarimo amesema TBS kwa kushirikiana na wadau wengine ilifanya uchunguzi wa kina, ikiwemo vipimo vya maabara na ufuatiliaji wa matumizi ya pombe katika jamii.
“Matokeo yalionesha kuwa bidhaa zote za pombe zilizofanyiwa uchunguzi ni salama. Changamoto kubwa iliyobainika ni matumizi holela ya pombe miongoni mwa wananchi,” amesisitiza.
Amefafanua kuwa matumizi holela ya pombe huweza kusababisha madhara ya kiafya, kijamii na kiuchumi, yakiwemo ajali, magonjwa ya moyo na ini, migogoro ya familia, kuporomoka kwa hali ya uchumi wa kaya na hata kupoteza maisha.
Katika kuhimiza udhibiti wa tatizo hilo, TBS imewataka wananchi kutumia bidhaa zenye alama ya uthibitisho wa ubora, kutoa taarifa wanapohisi uwepo wa bidhaa zisizo salama, na kuepuka shinikizo la rika katika unywaji wa pombe.

























0 Comments