Ticker

6/recent/ticker-posts

TPA YATUNUKIWA CHETI CHA HESHIMA KUTOKA KWA SHIRIKA LA FORODHA DUNIA (WCO).



Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Bw. Plasduce Mkeli Mbossa, ametunukiwa Cheti cha Heshima kwa usimamizi wake ikiwa ni kutambua na kuthamini mchango wangu wake mkubwa na utoaji huduma wa kipekee kwa jumuiya ya kimataifa ya Forodha, katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Forodha 2026.

Cheti hicho cha kimetolewa na Shirika la Forodha Duniani ( WCO) kwa niaba ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), katika maadhimisho yaliyofanyika tarehe 26 Januari, 2026, jijini Dar es Salaam, chini ya kaulimbiu isemayo:

“Forodha inalinda jamii kupitia umakini na uwajibikaji.”

Cheti hicho cha heshima kimetolewa ikiwa ni kuthamini huduma ya kipekee ya TPA chini ya usimamizi wa Bw. Mbossa na mchango mkubwa katika kuunga mkono na kuimarisha jumuiya ya kimataifa ya Forodha, hususan kupitia uboreshaji wa mifumo, taratibu na ushirikiano wa taasisi.

Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Forodha 2026 yalilenga kutambua na kuenzi mchango wa sekta ya forodha katika kukuza biashara halali, kulinda uchumi wa taifa, kuongeza makusanyo ya mapato ya serikali, pamoja na kuimarisha uwajibikaji na ushirikiano kati ya TRA na wadau wake wakuu, wakiwemo taasisi zinazosimamia bandari na biashara ya kimataifa.

Akizungumza kabla ya kukabidhi cheti hicho, Kamishna Mkuu wa TRA, Bw. Yusuph Juma Mwenda, aliipongeza TPA kwa ushirikiano wake wa karibu na wa muda mrefu na TRA, uliosaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha ufanisi wa shughuli za forodha bandarini, kurahisisha biashara na kuimarisha udhibiti wa mapato ya serikali.

Bw. Mwenda alieleza kuwa TPA imeendelea kuwa mdau muhimu na mfano wa kuigwa, kwa kuzingatia misingi ya weledi, uwajibikaji na uadilifu, huku ikiendelea kushirikiana kwa karibu na TRA katika utekelezaji wa maboresho ya mifumo na taratibu za forodha kwa manufaa ya taifa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Bw. Plasduce Mkeli Mbossa, ameishukuru TRA na Utawala wa Forodha wa Tanzania kwa kutambua mchango wake binafsi na wa taasisi ya TPA kwa ujumla, na kuahidi kuendelea kuimarisha ushirikiano uliopo ili kuongeza ufanisi wa bandari na kuchangia zaidi katika ukuaji wa uchumi wa nchi.

Bw. Mbossa amesema kuwa tuzo hiyo ni chachu kwa TPA kuendelea kuboresha huduma zake, kuimarisha matumizi ya teknolojia ya kisasa, pamoja na kudumisha misingi ya uwajibikaji, uwazi na uadilifu katika utoaji wa huduma za bandari na forodha.

Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Forodha yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kutathmini mafanikio ya sekta ya forodha, kuimarisha mahusiano na wadau wa biashara, pamoja na kuweka mwelekeo wa pamoja wa kuboresha mazingira ya biashara na maendeleo ya taifa kwa ujumla.







Post a Comment

0 Comments