Ticker

6/recent/ticker-posts

TUTATENGA FEDHA ZA KUJENGA BARABARA YA KUELEKEA KAMPASI YA MZUMBE TANGA - PROF. SHEMDOE

  

Na OWM - TAMISEMI, Mkinga

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI Mhe. Prof. Riziki Shemdoe amewaahidi wananchi wa Mkinga kuwa katika Bajeti ya Mwaka wa Fedha  2026/27 kupitia TARURA itatengwa fedha kwa ajili ya ujenzi wa   barabara yenye urefu wa kilomita 16 kwa kiwango cha changarawe, ambazo zitaunganisha Chuo cha Mzumbe Kampasi ya Tanga na barabara kuu ya TANROADS ili kuwezesha kampasi hiyo kufikika kwa urahisi.

Prof. Shemdoe ametoa ahadi hiyo leo Februari 15, 2026 baada ya Mhe. Waziri Mkuu Dkt. Mwigulu Mchemba, kumtaka Prof. Shemdoe kueleza mkakati wa kutatua changamoto ya ubovu wa barabara hiyo iliyowasilishwa na Mbunge wa Mkinga Mhe. Twaha Said Mwakioja na uongozi wa chuo, wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi katika Chuo Kikuu cha Mzumbe Kampasi ya Tanga.

"Mhe Waziri Mkuu ili kufika hapa Kampasi ya Chuo Kikuu cha Mzumbe kuna umbali wa kilomita 16 zinazoangukia TARURA kutoka ilipo barabara kuu ya TANROADS, katika bajeti mwaka wa fedha 2026/27 tutatenga fedha ya kujenga barabara hii kwa kiwango cha changarawe," amefafanua Prof. Shemdoe.

Akizungumzia barabara za ndani katika Kampasi hiyo  zenye urefu wa kilomita tano (5), Prof. Shemdoe amesema atazungumza na uongozi wa chuo ili kujua kipaumbele cha barabara za mzunguko wa ndani  ili kwa kuanzia zijengwe kilomita mbili kwa kiwango cha lami na kilomita  tatu zilizosalia  utawekwa utaratibu wa  namna ya kuzikamilisha.

Prof. Shemdoe ameendelea kueleza kuwa OWM TAMISEMI iko mstari wa mbele katika kuunga mkono kwa vitendo jitihada za Serikali za kuboresha miundombinu ya barabara kupitia TARURA, hususani katika kutekeleza maelekezo ya viongozi wakuu wa nchi wanayoyatoa pindi wanapokagua utekelezaji wa miradi mbalimbali  ya maendeleo.

Post a Comment

0 Comments