NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
WAKALA wa Vipimo (WMA) wameendelea kuendelea kutoa elimu kwa wafanyabiashara kuhusu matumizi sahihi ya mizani na vipimo badala ya kutumia nguvu katika utekelezaji wa sheria kwa wale ambao wanakaidi agizo.
Akizungumza katika kikao na wafanyabiashara wa masoko leo jijini Dar es Salaam Meneja wa WMA Mkoa wa Ilala, Muhono Nashon amesema lengo la elimu hiyo ni kujenga uelewa wa pamoja kabla ya maafisa wa vipimo kuanza ukaguzi mitaani.
Amefafanua kuwa wakala umejikita katika kutoa mafunzo kwa wafanyabiashara wanaotumia mizani ya aina mbalimbali ili kuhakikisha wanazingatia viwango vinavyotakiwa kisheria.
“Tunataka tunapokwenda kufanya ukaguzi tuwe tunaongea lugha moja na wafanyabiashara. Elimu ni muhimu kwa sababu wapo wapya sokoni na wengine hawafahamu taratibu za vipimo,” amesema Nashon.
Nashon aliongeza kuwa utoaji wa elimu ni endelevu, hasa katika mazingira ya masoko yanayopokea wafanyabiashara wapya mara kwa mara. Alisema baadhi ya changamoto hutokana na kutofahamu sheria, huku wengine wakifanya makosa kwa makusudi ili kujinufaisha.
Kwa upande wake, Katibu Msaidizi wa Soko la Ilala, Juma Bakari, aliiomba serikali kuhakikisha kunakuwa na usawa katika utekelezaji wa sheria za vipimo kuanzia mashambani hadi masokoni.
“Ni muhimu elimu hii ikaenda hadi kwa wakulima mashambani. Pia vyombo vya habari vitumike kuelimisha umma ili kila mtu afahamu viwango vinavyotakiwa,” amesema Bakari.
Bakari amesisitiza kuwa utekelezaji usio sawa unaweza kuibua malalamiko ya upendeleo au vitendo vya rushwa.
Nao baadhi ya wafanyabiashara wa jumla wameeleza changamoto wanazokutana nazo wanaposafirisha mazao kutoka mikoa mbalimbali kwenda Dar es Salaam. Walisema mara kadhaa hulipa faini njiani na wanapofika sokoni hukumbana tena na adhabu kwa madai ya kuzidisha ujazo wa magunia.
Mfanyabiashara wa viazi, Stella Mwakamboje, alisema tofauti ya vifungashio kama “mfuto” au “rumbesa” katika mikoa ya Mbeya na Njombe huleta mkanganyiko wa bei na ushindani usio sawa sokoni.
Amesema hali hiyo huathiri uwezo wa wafanyabiashara kurejesha mikopo wanayochukua kuendesha biashara.
Wafanyabiashara hao wameiomba serikali kuweka utaratibu mmoja wa kitaifa wa vifungashio na vipimo ili kuondoa tofauti hizo.
Wamesisitiza kuwa iwapo mizani itatumika rasmi, basi iwe kwa wote kuanzia mashambani hadi masokoni ili kuleta usawa wa kibiashara.
Mwenyekiti wa Soko la Ilala, Ali Mbiku, ameipongeza WMA kwa kutoa elimu hiyo, akisema itasaidia kulinda maslahi ya walaji na wafanyabiashara.
“Matumizi ya mizani yatasaidia mfanyabiashara kujua faida halisi badala ya kutegemea makadirio ya ujazo wa gunia,” amesema Mbiku.
Sambamba na hayo, Mbiku amelalamikia baadhi ya halmashauri kutoza faini kwa madai ya ukiukwaji wa vipimo wakati mamlaka ya kusimamia vipimo ipo kwa Wakala wa Vipimo pekee. Alisema ni muhimu mamlaka husika zishirikiane ili kuondoa migongano inayowaumiza wafanyabiashara.
0 Comments