Katika juhudi za kubadili ndoto za Watanzania kuwa uhalisia, TCB Bank imezindua kampeni mpya inayolenga kuimarisha ushirikiano wa karibu na wateja wake badala ya kutoa huduma za kifedha pekee.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika Machi 18, 2026 jijini Dar es Salaam, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Jema Msuya, amesema TCB imejipanga kuwa zaidi ya taasisi ya kifedha kwa kujikita kuwa mshirika wa kweli katika safari ya maendeleo ya mteja.
“Kwa kila azma, lengo au nia ya Mtanzania, tunatambua kuwa anastahili msaada wa stahiki. Ndiyo maana tunajitambulisha kama mshirika wa ukuaji, si tu benki,” amesema.
Ameeleza kuwa kampeni hiyo inaweka mkazo mkubwa katika uelewa wa mteja, akibainisha kuwa changamoto kubwa kwa wengi si kukosa ndoto, bali ni ukosefu wa msaada sahihi wa kifedha.
Kwa mujibu wa Msuya, TCB inaamini kuwa kumwezesha mjasiriamali mmoja kunachochea maendeleo ya jamii nzima.
Amesema kupitia huduma zake, benki hiyo inalenga kukuza biashara ndogo na za kati, kuimarisha ustawi wa jamii na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.
Amewahimiza Watanzania kuchukua hatua za kutimiza ndoto zao kwa kushirikiana na benki hiyo.
“Ndoto yako inaanzia kwako. Sisi tupo hapa kuhakikisha inakuwa uhalisia. Karibu tushirikiane kuijenga kesho bora,” amesisitiza.
Aidha, benki hiyo imeanza mpango maalum wa kuhuisha akaunti zisizotumika, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kurejesha uhusiano na wateja na kuwapatia huduma zenye tija zaidi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Masoko na Mawasiliano wa TCB, Alex Dwashi, amesema kampeni hiyo inalenga kugusa maisha ya Watanzania kwa kuwatambua na kuwaunga mkono katika safari ya kutimiza ndoto zao.
Amefafanua kuwa kuwa na ndoto pekee haitoshi, bali kunahitajika hatua madhubuti pamoja na msaada sahihi ili kuzifanya ziwe halisi.
Ametaja mifano ya wajasiriamali wanaoanzisha na kukuza biashara, wakulima wanaoongeza uzalishaji, pamoja na familia zinazowekeza katika elimu ya watoto wao, akisisitiza kuwa maendeleo katika maeneo hayo huongeza fursa kwa jamii nzima.
Ameongeza kuwa kupitia kampeni hiyo, TCB inalenga kujenga uhusiano wa karibu zaidi na wateja wake kwa kuwauliza swali kuu, “Ndoto yako ni nini?”, ili iweze kutoa suluhisho mahsusi kulingana na mahitaji ya kila mmoja.
Aidha, amesema benki hiyo imejipanga kuhudumia makundi mbalimbali ikiwemo wafanyabiashara, wajasiriamali, wakulima na familia, huku ikipanua huduma zake katika maeneo ya uwekezaji na bima.
0 Comments