NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
MTANDAO wa Jinsia Tanzania (TGNP), kwa kushirikiana na taasisi ya Sightsavers na YOWDO, umeandaa jukwaa maalumu la vijana na watu wenye ulemavu kwa lengo la kujadili fursa, changamoto na mikakati ya kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya uchumi wa nchi.
Akizungumza leo Machi 19, 2026 jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Programu wa TGNP, Bi. Anna Sangai, amesema jukwaa hilo linafanyika ikiwa ni sehemu ya kuelekea kilele cha Maadhimisho ya Mwezi wa Wanawake, likilenga kuwapa vijana nafasi ya kujadili masuala yanayowahusu na kupata uelewa mpana zaidi.
Amesema jukwaa hilo pia linatoa fursa kwa vijana kuuliza maswali, kubadilishana mawazo na kujifunza kuhusu haki, fursa na wajibu wao katika kuchangia maendeleo ya taifa.
Kwa mujibu wa takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, idadi ya watu wenye ulemavu imeongezeka kutoka asilimia 9.3 mwaka 2012 hadi asilimia 11.2 mwaka 2022, hali inayoonesha umuhimu wa kuongeza juhudi za ujumuishaji katika mipango ya maendeleo.
“Mchakato huu unaonesha wazi kuwa taifa linaelekea kwenye kuhakikisha ujumuishaji katika fursa, mipango na bajeti kwa watu wote, hususan vijana wenye ulemavu,” amesema Sangai.
Ameongeza kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, katika nguzo ya uchumi imara, jumuishi na shindani, inalenga kuwa na mfumo wa kifedha unaowezesha wananchi wote kushiriki kikamilifu, huku ukitoa kipaumbele kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Kwa upande wake, mmoja wa washiriki wa jukwaa hilo, Ridhiwani Burhani, amesema anatarajia kuona wanawake, hususan wenye ulemavu, wakipewa nafasi kubwa zaidi katika nyanja zote za maendeleo kutokana na uwezo wao mkubwa.
Naye Maimuna Saidi amesema matarajio yake ni kuona kundi la watu wenye ulemavu, hasa wanawake, likinufaika zaidi na fursa mbalimbali ifikapo mwaka 2050, akieleza kuwa juhudi za serikali zimeanza kuleta mabadiliko kupitia elimu inayotolewa kwa jamii.
Akizungumza katika jukwaa hilo, Afisa Mradi wa Sightsavers, Sabina Maheke, amesema mjadala huo utasaidia kuweka mikakati madhubuti ya kuwasaidia vijana wenye ulemavu, hasa wanawake, kupata fursa za ajira na kujikwamua kiuchumi.
0 Comments