Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mahmoud Thabit Kombo (Mb) amewasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mpango wa Bajeti wa mwaka 2025/2026 na mpango wa bajeti wa mwaka wa Fedha 2026/2027 kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ulinzi na Usalama (NUU) jijini Dodoma.
Akiwasilisha taarifa hiyo, Balozi Kombo alieleza hatua mbalimbali zilizofikiwa na wizara katika kutekeleza majukumu yake, ikiwemo kuimarisha diplomasia ya uchumi, kulinda maslahi ya Taifa na kukuza ushirikiano wa uwili, kikanda na kimataifa.
Katika taarifa hiyo, Mhe. Balozi Kombo alibainisha mafanikio yaliyopatikana kupitia ushiriki wa Tanzania katika majukwaa ya kimataifa na kikanda na juhudi za kuvutia uwekezaji na kupanua fursa za biashara kwa Watanzania.
Alisisitiza umuhimu wa kuendelea kuelimisha wadau kuhusu fursa zitokanazo na uhusiano wa kimataifa na hivyo kuleta tija ya diplomasia ya uchumi nchini.
Kuhusu mpango wa bajeti wa mwaka 26/27, Waziri Kombo alieleza kuwa vipaumbele vya Wizara vitaendelea kutekelezwa kwa kuzingatia miongozo ya kitaifa, kikanda na kimataifa, Sera ya Mambo ya Nje; Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050; Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2050; Mpango wa Nne wa Taifa waMaendeleo wa Miaka Mitano (26/27 - 30/31); Mpango wa Maendeleo wa Zanzibar(2021 – 2026); Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya Uchaguzi ya 2025; Mkataba wa Uanzishwaji wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wa mwaka 1999; Mkataba wa Uanzishwaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika wa mwaka 1992; Ajenda ya Mwaka 2030 ya Umoja wa Mataifa kuhusu Maendeleo Endelevu; Ajenda ya Mwaka 2063 ya Umoja wa Afrika; Dira ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika ya Mwaka 2050; Dira ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Mwaka 2050; na mikataba mingine ya Kikanda na Kimataifa.
Alitaja vipaumbele vya Wizara kwa mwaka wa fedha 2026/2027 kuwa ni Kuendelea kuimarisha uratibu na ushirikiano wa uwili, kikanda na kimataifa; Kuratibu utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje hususan utekelezaji wa diplomasia ya uchumi; Kulinda Taswira, heshima na kutetea maslahi ya Taifa letu katika nyanja ya kimataifa; na Kuboresha mazingira ya utendaji kazi kwa watumishi wa Wizara, kuimarisha utawala bora na rasilimali watu pamoja na kutekeleza miradi ya maendeleo ya Wizara na taasisi zake.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ulinzi na Usalama Mhe. Najma Giga (Mb) aliipongeza Wizara kwa uwasilishaji wa taarifa hiyo kwa ufasaha.
Alieleza kuwa Kamati hiyo itaendelea kushirikiana na Wizara ili iendelee kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kwamba kukiwa na jambo linalowahitaji wawasiliane ili kujadili kwa pamoja na kuona jinsi ya kulitanzua kwa pamoja










0 Comments