Ticker

6/recent/ticker-posts

COASTAL HIGH SCHOOL YAJIPANGA KUENDANA NA MABADILIKO YA SAYANSI NA TEKNOLOJIA DUNIANI





Na Oscar Assenga, Tanga

Katika kuendana na kasi ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia duniani, Shule ya Sekondari Coastal High School imetangaza mpango kabambe wa kuanzisha programu ya Akili Unde (Artificial Intelligence - AI) ifikapo Januari 2027.

Mpango huo unalenga kuwajengea wanafunzi ujuzi wa kisasa utakaowawezesha kushindana katika soko la ajira la Kimataifa.

Akizungumza wakati wa mahafali ya Kidato cha Sita yaliyofanyika jijini Tanga, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo,Isack Dastan Kifwete alisema kuwa tayari wameanza kuchukua hatua muhimu kuelekea utekelezaji wa mpango huo.


Miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na kufanikisha upatikanaji wa huduma ya intaneti kupitia Kampuni ya TTCL, pamoja na kuwepo kwa mtaalamu wa TEHAMA shuleni hapo.

Hata hivyo, alibainisha kuwa bado kuna changamoto kadhaa zinazokwamisha utekelezaji wa mpango huo kwa ufanisi unaohitajika.



Alizitaja changamoto hizo ni pamoja na uhaba wa vifaa muhimu kama kompyuta za kisasa, ubao janja (smart board), pamoja na miundombinu ya chumba maalumu kitakachotumika kufundishia programu ya AI.



Mbali na hilo, shule pia ina mpango wa kuanzisha programu ya Habari na Mawasiliano ya Umma, unaolenga kuwajengea wanafunzi uwezo wa uandishi wa habari, mawasiliano, pamoja na matumizi ya teknolojia za kisasa katika tasnia ya habari.

Tayari maandalizi ya awali, ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya studio, yameanza kufanyika.



Pamoja na jitihada hizo, Mwalimu Mkuu alieleza kuwa shule bado inahitaji vifaa muhimu ili kukamilisha studio hiyo.

Vifaa vinavyohitajika ni pamoja na kamera za kisasa, meza ya matangazo, vifaa vya kuzuia kelele, vinasa sauti, vipaza sauti pamoja na kompyuta zenye uwezo wa kisasa.



Aidha, alitaja changamoto nyingine zinazoikabili shule kuwa ni pamoja na baadhi ya wazazi kushindwa kulipa ada kwa wakati kutokana na hali ngumu ya kiuchumi, pamoja na ushiriki mdogo wa wazazi na walezi katika masuala ya kitaaluma na malezi ya wanafunzi.

Kutokana na hali hiyo, uongozi wa shule umetoa wito kwa wadau mbalimbali kujitokeza kusaidia jitihada hizo ikiwemo kuwaomba wadau msaada wa vifaa kwa ajili ya kuanzisha studio ya habari, pamoja na kuunganishwa na taasisi au watu binafsi wanaoweza kusaidia upatikanaji wa kompyuta za kisasa.



Kwa ujumla, mpango huu unaonesha dhamira ya dhati ya shule katika kuwajengea wanafunzi msingi imara wa elimu ya kisasa ili kuwaandaa kukabiliana na dunia inayoendeshwa na teknolojia kwa kasi kubwa.

Awali, akizungumza katika mahafali hayo,Mgeni rasmi ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Chumbuni Zanzibar (CCM), Ussi Salum Pendeza, alisema kuwa atashirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha baadhi ya changamoto zinapatiwa ufumbuzi kwa haraka.



Alisema kuwa ataanza mwenyewe kuchangia upatikanaji wa baadhi ya vifaa muhimu, ikiwemo kompyuta za kisasa na ubao janja, sambamba na kuhamasisha wadau wengine kushiriki.

“Katika hili la ubao janja na baadhi ya kompyuta, nitaanza mimi mwenyewe. Pia nitahakikisha michango inapatikana na kuwashirikisha wengine. Nachukua nafasi hii kuwashukuru walimu na Bodi ya Shule ya Coastal kwa ushirikiano wao katika kuhakikisha shule inafanya vizuri na matokeo yanakuwa mazuri,” alisema.



Ussi, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Shule hiyo, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), mfanyabiashara na Mkurugenzi wa Taasisi ya Pendeza Foundation, alisema anajivunia kuiongoza shule hiyo na ameahidi kuendelea kuisimamia ili iweze kufanya vizuri zaidi na kujulikana kitaifa.





























Post a Comment

0 Comments