Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Richard Muyungi (kushoto) akishiriki Mkutano wa 12 wa Kikanda wa Afrika kuhusu ‘Agenda 2030 yaMaendeleo Endelevu’ na ‘Agenda 2063 ya Afrika Tuitakayo’, uliofunguliwa Aprili28, 2026 jijini Addis Ababa, Ethiopia.
**********
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inashiriki Mkutano wa 12 wa Kikanda wa Afrika kuhusu ‘Agenda 2030 ya Maendeleo Endelevu’ na ‘Agenda 2063 ya Afrika Tuitakayo’, uliofunguliwa Aprili 28, 2026 jijini Addis Ababa, Ethiopia.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Richard Muyungi ni miongoni mwa viongozi wanaoshiriki katika mkutano huo ulioandaliwa na Tume ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa kwa Afrika (UNECA).
Mkutano huo umefunguliwa na Katibu Mtendaji wa Tume ya Umoja wa Mataifa ya Uchumi kwa Afrika Balozi Claver Gatete.
Katika hotuba yake alieleza kuwa Tume ya Uchumi ya Afrika na Umoja wa Mataifa utaendelea kuunga mkono Nchi wanachama kupitia ushauri wa kisera katika kujenga uwezo na ushirikiano ambao utatoa matokeo yanayoweza kupimika.
Aidha, mkutano huo unaohusisha Nchi Wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) na Wadau unalenga kufanya mapitio ya maendeleo yaliyofikiwa katika utekelezaji wa malengo ya maendeleo endelevu.
Pia, mkutano huo utafanya tathmini ya kina ya maendeleo katika maeneo mbalimbali ikiwemo ya Maji Safi na Usafi, Nishati Nafuu na Safi na Viwanda, Ubunifu na Miundombinu.
Masuala mengine yatakayogusiwa kwenye mkutano ni pamoja na hatua za mageuzi na uratibu ili kuharakisha utekelezaji wa Mpango wa Pili wa Utekelezaji wa Miaka 10 wa Ajenda 2063 pamoja na Malengo ya Maendeleo Endelevu kati ya sasa na 2030,
Halikadhalika, washiriki wa mkutano watapokea mawasilisho mbalimbali yakiwemo Ripoti ya Maendeleo Endelevu ya Afrika, 2026, kwa kuzingatia hatua za kuleta mageuzi na uratibu kwa ajili ya utekelezaji jumuishi na wa haraka wa ajenda hizo mbili.
Mkutano huo unawakutanisha washiriki kutoka mataifa mbalimbali wakiwemo viongozi, wataalamu na wawakilishi wa vijana, unatarajiwa kuhitimishwa Aprili 30, 2026.

0 Comments