
Na Mwandishi Wetu
Kampuni ya Taifa Gesi imeendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi sahihi na salama ya gesi, sambamba na kuhamasisha usalama mahali pa kazi katika maadhimisho ya Wiki ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi Duniani.
Akizungumza katika viwanja vya Shule ya Msingi Mji Mwema, Njombe, Mtaalamu wa Masuala ya Afya, Mazingira, Usalama na Ulinzi Mahali pa Kazi kutoka Taifa Gesi, Aurelius Marcus Mdemu, alisema kampuni hiyo imeshiriki maadhimisho hayo yanayoanza Aprili 24 hadi 29, 2026 kwa lengo la kutoa elimu kwa wateja na jamii kwa ujumla.

Alisema kupitia banda lao, wanaonesha vifaa mbalimbali vinavyotumika kazini ili kuimarisha usalama wa wafanyakazi, pamoja na kutoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya gesi na faida zake. Aidha, alieleza kuwa wanajitahidi kuondoa hofu na dhana potofu zilizopo miongoni mwa watumiaji wa gesi.
“Tunawaonesha wananchi namna Taifa Gesi inavyoweka kipaumbele kwenye usalama wa wafanyakazi, ikiwa ni pamoja na matumizi ya vifaa kinga vinavyotakiwa kutumika muda wote wakiwa kazini,” alisema Mdemu.


Kwa upande wake, Afisa Masoko wa Chapa wa Taifa Gesi, Santina Ngaponda, alisema maonyesho hayo yameandaliwa na OSHA, yalianza Aprili 24 na yanatarajiwa kufikia kilele chake Aprili 29 mwaka huu.
Ngaponda aliwahimiza wakazi wa Njombe na maeneo ya jirani kutembelea banda la Taifa Gesi ili kupata elimu kutoka kwa wataalamu wa usalama, kujifunza matumizi sahihi ya gesi, pamoja na kuona vifaa vya usalama vinavyotumika kazini na umuhimu wake.

Aidha, aliongeza kuwa kampuni hiyo inatoa punguzo maalum la bei ya gesi na vifaa vyake, pamoja na zawadi mbalimbali kwa wateja watakaotembelea banda hilo.

Naye Meneja Mauzo wa Kanda ya Nyasa wa Taifa Gesi, Arnold Salewa, alisema wanaendelea kutumia maonyesho hayo kutoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya nishati safi pamoja na kuuza bidhaa zao kwa bei ya promosheni.
Alisema kanda hiyo inajumuisha mikoa ya Njombe, Iringa na Ruvuma, na kwamba pia wanatoa fursa kwa wananchi wanaotaka kuwa mawakala wao, kwa kuwapatia elimu ya biashara na usimamizi salama wa mitungi ya gesi.

Salewa alisisitiza kuwa Taifa Gesi ipo mstari wa mbele kuhakikisha kaya, migahawa na taasisi mbalimbali zinaanza kutumia nishati safi ya kupikia kwa gharama nafuu, ili kupunguza athari za matumizi ya mkaa na kuni kwa mazingira na afya za Watanzania.
Aliongeza kuwa mwitikio wa wananchi umekuwa mkubwa, huku Taifa Gesi ikiendelea kuwa chaguo sahihi kwa watumiaji wengi nchini.
0 Comments