Ticker

6/recent/ticker-posts

TUKAI :TUNAYO AKIBA YA KUTOSHA DAWA NA VIFAA TIBA NCHINI

*Awatoa hofu Watanzania wanaohofia upungufu wa dawa kutokana na mzozo mashariki ya kati

Na Said Mwishehe, Dodoma

MKURUGENZI Mkuu wa Bohari ya Dawa(MSD) Mavere Tukai amewahakikishia Watanzania kuwa upatikanaji wa dawa na vifaa tiba nchini uko imara kwani kuna akiba ya kutosha kwa kipindi cha zaidi ya miezi sita, licha ya kuendelea kwa mzozo wa Mashariki ya Kati.

Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Mavere Tukai, ameyasema hayo katika kikao kazi kilichohusisha wahariri na waandishi wa habari walipokutana kujadili masuala mbalimbali katika sekta ya afya na hasa mchango wa MSD katika kuendeleza jitihada za kuhakikisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba unakuwa wa uhakika nchini.

Hivyo ametumia kikao hicho kuwatoa wasiwasi miongoni mwa wananchi kuhusu uwezekano wa kupungua kwa dawa na vifaa tiba, hasa kutokana na athari zinazoweza kusababishwa na mvutano wa kijeshi kati ya Marekani na Iran.

“MSD imejipanga vyema kuhakikisha upatikanaji endelevu wa bidhaa hizo muhimu na tayari kuna tathmini inayoendelea kufanywa na timu maalumu ya wataalamu ili kubaini hatari zinazoweza kujitokeza na kuweka mikakati madhubuti ya kukabiliana nazo.”

Mkurugenzi Mkuu ameongeza juhudi zinaendelea kuimarishwa, hasa katika kuhakikisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba vinavyoagizwa kutoka nje ya nchi hauathiriki na mabadiliko ya hali ya usalama na uchumi wa kimataifa.

“Serikali itaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa hali hiyo ili kuhakikisha huduma za afya nchini haziathiriki na wananchi wanaendelea kupata huduma bora bila usumbufu.

Post a Comment

0 Comments