Ticker

6/recent/ticker-posts

RAIS SAMIA AMPATIA TUZO PROFESA NDUNGURU KWA KUPAISHA MAPATO TPHPA


Na Mwandishi Wetu, Njombe.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, juzi katika maadhimisho ya Mei Mosi kitaifa, alimpatia tuzo ya Mfanyakazi Hodari, ikiwemo cheti na zawadi, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA), Profesa Joseph Ndunguru.

Profesa Ndunguru anatoka Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia, Taasisi za Habari, Vyuo vya Ufundi Stadi na Taasisi za Utafiti (RAAWU). Alijiunga na TPHPA mwaka 2023 na tangu wakati huo ameifanya taasisi hiyo kuwa ya mfano barani Afrika kupitia maboresho makubwa ya kiutendaji.

Miongoni mwa mafanikio hayo ni kuongeza uwezo wa kuchambua viuatilifu, kuboresha maabara kuwa za kisasa, pamoja na kuziunganisha katika mfumo mmoja unaosomana. Mfumo huo unahusisha ofisi 47 zilizopo katika mipaka ya Tanzania zinazoshughulikia upimaji na uingizaji wa viuatilifu, hali iliyoongeza ufanisi na mapato kutoka shilingi bilioni 14 mwaka 2023 hadi kufikia bilioni 69 ndani ya miezi minane tu kuanzia Julai 2025 hadi Februari mwaka huu.

Akizungumza katika sherehe hizo, Rais Samia aliwapongeza wafanyakazi hodari waliotunukiwa tuzo pamoja na wafanyakazi wote nchini kwa mchango wao katika kukuza uchumi wa taifa, huku akiahidi kuendelea kuboresha maslahi yao.

“Chapeni kazi, Serikali inatambua mchango wenu. Kadri hali ya uchumi inavyozidi kuimarika, tutaendelea kuboresha maslahi yenu. Pia tunaendelea kulipa malimbikizo ya madai na kutafuta fursa zaidi za ajira zenye staha ndani na nje ya nchi,” alisema.

Kwa upande wake, Profesa Ndunguru alisema ushindi huo umetokana na ushirikiano mkubwa kati ya TPHPA na Serikali pamoja na mshikamano wa wafanyakazi wake katika kutekeleza maelekezo ya Rais.

“Mimi ni kiongozi tu, lakini mafanikio haya ni ya pamoja. Ndani ya miaka mitatu tumefikia hatua ya kupokea watafiti na wanasayansi kutoka nchi mbalimbali za Afrika kuja kujifunza kutoka kwetu,” alisema.

Aliongeza kuwa TPHPA sasa imepunguza adha kwa wafanyabiashara wa mazao ya kilimo waliokuwa wakilazimika kupima bidhaa zao nje ya nchi kwa ajili ya masoko ya kimataifa, kwani huduma hizo zinapatikana ndani ya Tanzania na maabara zake zinatambulika kimataifa.

Awali, mazao mengi yalikuwa yakipelekwa kupimwa katika nchi jirani kabla ya kusafirishwa nje, lakini sasa yanapimwa hapa nchini na kupata ithibati inayokubalika kimataifa.

Akizungumzia mchango kwa wakulima, alisema mamlaka hiyo imekuwa ikiwasaidia kuzalisha mazao bora yasiyo na mabaki ya viuatilifu na kuwatafutia masoko ya kimataifa, hasa kwa mazao ya kimkakati.

Alitaja kuwa kampuni 16 za mazao ya parachichi na viazi mviringo zimepatiwa masoko nchini China, huku wakulima wadogo wa viazi wakisaidiwa kusafisha mazao yao hapa nchini kabla ya kuyasafirisha nje.

Profesa Ndunguru alisema pia ujenzi wa maabara zaidi unaendelea katika makao makuu ya TPHPA mkoani Arusha, pamoja na mipango ya kujenga maabara nyingine katika mji wa Makambako ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wakulima.

Aidha, alibainisha kuwa TPHPA inakusudia kujenga kituo cha kuhifadhi mbegu za asili zaidi ya 10,000 kwa ajili ya matumizi ya wakulima na watafiti, huku uwezo wa sasa wa kuchambua sampuli ukifikia 2,000 kwa wiki.

Katika hatua nyingine, aliahidi kushirikiana na Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania (JOWUTA) kuwajengea uwezo wanahabari kuhusu shughuli za mamlaka hiyo, pamoja na kusaidia kufichua biashara haramu ya viuatilifu visivyoidhinishwa.

Naye Mwenyekiti wa JOWUTA Taifa, Mussa Juma, alimpongeza Profesa Ndunguru na wafanyakazi wa TPHPA kwa kazi nzuri wanayoifanya, huku akiishukuru mamlaka hiyo kwa kuwa mdhamini wa tuzo za wanahabari hodari mwaka 2026.

Post a Comment

0 Comments