Mratibu wa TGNP, Anna Sangai akizungumza katika mjadala wa uchambuzi wa Bajeti ya Taifa ulioandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP).
***
Wadau wa maendeleo wameitaka Serikali kuhakikisha Bajeti ya Taifa ya mwaka 2026/2027 inatekelezwa kwa kuzingatia usawa wa kijinsia ili kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Kuli hiyo ilitolewa jana katika mjadala wa uchambuzi wa Bajeti ya Taifa ulioandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kupitia jukwaa la Kijiwe cha Kahawa, lililowakutanisha wadau wa maendeleo, wanaharakati, wataalamu wa uchumi na viongozi wa serikali za mitaa.
Mratibu wa TGNP, Anna Sangai, alisema bajeti yenye mrengo wa kijinsia ni muhimu katika kuhakikisha wanawake, vijana, watoto na makundi mengine yaliyo pembezoni yanapata fursa sawa za maendeleo na kushiriki kikamilifu katika uchumi wa taifa.
Alisema TGNP imeendelea kuwa jukwaa la wananchi kuwasilisha vipaumbele vyao kupitia mijadala ya bajeti, huku ikiitaka Serikali kuelekeza uwekezaji zaidi katika huduma za maji, afya, elimu na uwezeshaji wa wanawake na vijana.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Utafiti na Maendeleo wa Taasisi ya WAJIBU, Kadeghe Karoli Kadeghe, alisema bajeti ya mwaka huu ni ya kihistoria kwa kuwa ndiyo hatua ya mwanzo ya utekelezaji wa Dira ya Taifa a Maendeleo 2050.
Mkurugenzi wa Utafiti na Maendeleo wa Taasisi ya WAJIBU, Kadeghe Karoli Kadeghe,akizungumza kando ya mjadala wa uchambuzi wa Bajeti ya Taifa ulioandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kupitia jukwaa la Kijiwe cha Kahawa.Alisema ili kufikia malengo hayo, kuna haja ya kuimarisha usimamizi wa fedha za umma pamoja na kuyafanyia kazi mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ili kuongeza uwajibikaji na tija ya matumizi ya fedha za wananchi.
Naye Mchumi Daraja la Pili wa Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga, Charles Daudi, alisema halmashauri hiyo imejipanga kuhakikisha mipango na bajeti zake zinazingatia usawa wa kijinsia katika sekta za elimu, kilimo na uvuvi.
Daudi alisema miongoni mwa mipango iliyowekwa ni kutenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa taulo za kike kwa wanafunzi wa kike, kuanzisha chumba maalumu cha kujisitiri kwa wanafunzi wanapokuwa kwenye hedhi na kuhakikisha mikopo ya asilimia 10 inawanufaisha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwa usawa.


Wadau wa maendeleo, wanaharakati, wataalamu wa uchumi na viongozi wa serikali za mitaa wakifuatilia mjadala wa uchambuzi wa Bajeti ya Taifa ulioandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kupitia jukwaa la Kijiwe cha Kahawa.



0 Comments