Shirika la Masoko ya Kariakoo limewataharisha wananchi wanaotaka maeneo ya kufanya biashara katika Soko Kuu la Kariakoo kuepuka matapeli wanaowataka kuwapa fedha ili wapatiwe maeneo ya kufanya biashara katika soko hilo.
Rai hiyo imetolewa na Meneja Mkuu wa shirika hilo CPA. Ashraph Abdulkarim na kuongeza kuwa maeneo katika soko hilo yanatolewa bila mfanyabiashara kulipa malipo ya ziada, kwakuwa malipo yote yanayotakiwa kulipwa yapo kwa mujibu ya sheria, kanuni na taratibu za nchi.
“Kupata eneo katika soko letu la Kariakoo huhutaji kumjua mtu, kulipa kilemba wala kwenda kwa dalali njoo kwenye ofisi zetu za shirika, kama maeneo yapo utaelekezwa utaratibu wa kufuata ili uweze kupatiwa kwa mujibu wa utaratibu uliopo” amebainisha CPA. Abdulkarim
Aidha, CPA. Abdulkarim amewataharisha wale wote wanaowarubuni wafanyabiashara kuwa watawapa maeneo ya kufanyia biashara ili wapate fedha waache tabia hizo kwani shirika halitasita kuchukua hatua za kisheria pale watakapobainika kujihusisha na vitendo hivyo.
Pia, amewataka wafanyabiashara waliopangishiwa maeneo kulipa kodi zao kwa wakati ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza na kwa wale waliopewa notisi ya kufungua biashara zao wafanye hivyo kwani shirika lipo mbioni kuchukua maeneo hayo endapo hayataendelezwa.
Ikumbukwe kuwa Mei 21, 2026 Shirika la Masoko lilitoa tangazo kwa kwa wafanyabiashara kuendeleza maeneo yao ndani ya siku 14 kuanzia tarehe hiyo na kwa wale ambao hawataendeleza maeneo yao yatachukuliwa na kupewa wafanyabiashara wenye uhitaji.

0 Comments