Ticker

6/recent/ticker-posts

PROF. SHEMDOE AWATAKA WALIMU KUONGEZA UBUNIFU KATIKA UFUNDISHAJI

-Walimu 35 walioshinda tuzo za ufundishaji kupatiwa viwanja

WALIMU nchini wamehimizwa kuendelea kufanya kazi kwa bidii, kujituma na kutumia mbinu bunifu za ufundishaji ili kuimarisha ubora wa elimu na kuchangia maendeleo ya taifa, huku walimu 35 walioibuka washindi katika Shindano la Taifa la Stadi za Ufundishaji wakielekezwa kupatiwa viwanja karibu na maeneo yao ya kazi kama sehemu ya motisha.

Akizungumza Juni 6, 2026 jijini Dar es Salaam katika hafla ya utoaji wa zawadi kwa washindi wa shindano hilo kwa walimu wa elimu ya awali, msingi na sekondari, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Prof. Riziki Shemdoe, amesema walimu wana mchango mkubwa katika kuwalea na kuwaandaa wanafunzi kuwa wananchi wenye maarifa, stadi na maadili mema yanayohitajika katika jamii.

Prof. Shemdoe amesema Serikali itaendelea kuthamini mchango wa walimu kwa kuweka mazingira bora ya kazi na motisha mbalimbali zinazolenga kuongeza ufanisi katika ufundishaji na ujifunzaji.

Aidha, amewataka walimu kuendelea kutumia mbinu za kisasa na bunifu katika ufundishaji ili kuwajengea wanafunzi uwezo wa kufikiri kwa kina, kubuni na kukabiliana na changamoto za dunia ya sasa.

Amesema tuzo hizo zinalenga kuhamasisha ubora, uwajibikaji, ubunifu na kujituma katika kazi za kufundisha, akisisitiza kuwa maendeleo ya taifa yanategemea kwa kiasi kikubwa ubora wa rasilimali watu inayozalishwa kupitia mfumo wa elimu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo, Husna Sekiboko, amesema mafanikio katika sekta ya elimu yanahitaji ushiriki wa wadau wote, wakiwemo wazazi, walimu, wanafunzi na viongozi wa jamii.

Amesema maboresho yanayoendelea katika mifumo ya uongozi na utawala yanalenga kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma za elimu na kuimarisha matokeo ya kujifunza kwa wanafunzi.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Dkt. Aneth Komba, amesema shindano la Taifa la Stadi za Ufundishaji la mwaka 2026 ni la nne kwa walimu wa elimu ya awali na msingi na la pili kwa walimu wa elimu ya sekondari, likihusisha halmashauri zote 184 za Tanzania Bara.

Amesema kwa upande wa elimu ya awali, shindano hilo limejikita katika kuimarisha umahiri wa ufundishaji wa stadi za kusoma, hususan sauti za herufi ambazo zimekuwa changamoto kwa baadhi ya wanafunzi katika kuzitamka na kuzitumia kwa usahihi katika kuunda silabi na maneno.

“Lengo la shindano hili ni kusaidia kutatua changamoto za ufundishaji na ujifunzaji wa stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) ili kuhakikisha wanafunzi wanazimudu stadi hizo muhimu wanapofikia Darasa la Tatu. Eneo hili la ushindani linaunga mkono maono ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha watoto wote wanasoma kwa ufasaha wanapofikia Darasa la Tatu,” amesema Dkt. Komba.

Ameeleza kuwa maandalizi ya shindano hilo yalihusisha uchambuzi wa matokeo ya wanafunzi kupitia taarifa za Baraza la Mitihani la Tanzania pamoja na maeneo mapya yaliyoingizwa katika mtaala ili kubaini maeneo yanayohitaji kupewa kipaumbele.

Kwa mujibu wa Dkt. Komba, walimu walitakiwa kuandaa andalio la somo, kujirekodi wakifundisha kwa muda wa dakika 10 hadi 15 na kupakia video pamoja na andalio hilo katika mfumo wa kidijitali wa National Teaching Skills Competition System kwa ajili ya tathmini.

Jumla ya walimu 3,153 walijisajili katika mfumo huo, huku walimu 1,263 sawa na asilimia 40 wakifanikiwa kupakia video zao kwa ajili ya tathmini katika ngazi ya halmashauri.

Amesema tathmini ilifanyika katika ngazi tatu ambazo ni halmashauri, mkoa na taifa kwa kuzingatia vigezo mbalimbali ikiwemo ubora wa maudhui, mtiririko wa somo, matumizi ya mbinu shirikishi, matumizi ya TEHAMA, matumizi ya zana za kufundishia, ukuzaji wa stadi za karne ya 21 na matumizi ya upimaji endelevu katika mchakato wa ufundishaji na ujifunzaji.

Katika mchujo wa shindano hilo, video 751 zilifanikiwa kuingia ngazi ya mkoa kutoka video 1,263 zilizotathminiwa katika ngazi ya halmashauri. Kati ya hizo, video 232 zilichaguliwa kuingia ngazi ya taifa.

Post a Comment

0 Comments