Dar es Salaam, Juni 5, 2026
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limekabidhi rasmi Karakana ya kuongeza mfumo wa matumizi ya gesi asilia Iliyoshindiliwa kwenye vyombo vya usafiri (CNG Conversion Workshop) kwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), hatua inayotarajiwa kuimarisha matumizi ya nishati safi nchini pamoja na kukuza ujuzi wa kitaalamu katika teknolojia ya gesi asilia.
Makabidhiano hayo yamefanyika leo katika eneo jijini Dar es Salaam, ambapo TPDC iliwakilishwa na Mkurugenzi wa Idara ya Mipango na Uwekezaji, Bw.Derick Moshi, kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC. Kwa upande wa UDSM, karakana hiyo ilipokelewa na Naibu Mkuu wa Chuo Prof. Bernadeta Kilian.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Bw. Derick Moshi alisema kuwa ujenzi wa karakana hiyo ni sehemu ya jitihada za TPDC katika kuunga mkono mkakati wa Serikali wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi na nafuu kwa wananchi.
“Kukamilika na kukabidhiwa kwa karakana hii ni hatua muhimu katika kukuza matumizi ya gesi asilia Iliyoshindiliwa (CNG) nchini. Mbali na kutoa huduma za kuongeza mifumo ya CNG kwenye magari, karakana hii itatumika kujenga wataalamu wazalendo kupitia mafunzo ya vitendo kwa wanafunzi wa uhandisi wa UDSM,” alisema Bw. Moshi.
Aliongeza kuwa mradi huo umegharimu shilingi bilioni 1.52 za Kitanzania na ni sehemu ya utekelezaji wa makubaliano ya ushirikiano kati ya TPDC na UDSM yaliyowekwa kupitia Mkataba wa Upangishwaji Ardhi uliosainiwa mwaka 2022.
Kwa mujibu wa Bw. Moshi, karakana hiyo ina vifaa vya kisasa vinavyowezesha ufungaji wa mifumo ya CNG kwenye vyombo vya usafiri, ukaguzi wa usalama wa mifumo hiyo pamoja na matengenezo yake, hatua itakayochangia kupunguza gharama za matumizi ya nishati kwa watumiaji wa magari nchini.
Kwa upande wake, Prof. Bernadeta Kilian aliishukuru TPDC kwa kutekeleza ahadi yake ya kujenga na kukabidhi karakana hiyo, akieleza kuwa miundombinu hiyo itakuwa kichocheo muhimu katika maendeleo ya elimu, utafiti na ubunifu wa teknolojia za nishati nchini.
“Kupokea karakana hii ni hatua kubwa kwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Miundombinu hii itawapa wanafunzi wetu nafasi ya kupata mafunzo ya vitendo yanayokidhi mahitaji ya soko la ajira na wakati huo huo kusaidia maendeleo ya sekta ya nishati nchini,” alisema Prof. Kilian
Alisisitiza kuwa UDSM itaendelea kushirikiana na TPDC katika tafiti, ubunifu na maendeleo ya teknolojia zinazochangia matumizi bora ya rasilimali za gesi asilia kwa manufaa ya Taifa.
Karakana hiyo imejengwa ndani ya eneo la Kituo Mama cha kujaza gesi asilia (CNG Mother Station) kilichopo UDSM na inatarajiwa kuwa kituo muhimu cha utoaji huduma za CNG pamoja na mafunzo ya kitaalamu kwa wanafunzi na wadau wa sekta ya usafiri.
Kupitia uwekezaji huo, TPDC inaendelea kutekeleza dhamira ya Serikali ya kuhamasisha matumizi ya Nishati Safi, salama na nafuu, sambamba na kuongeza ushiriki wa taasisi za elimu ya juu katika maendeleo ya sekta ya nishati nchini.













0 Comments