Ticker

6/recent/ticker-posts

WAZIRI SANGU: MAONESHO YA AJIRA TANZANIA - CHINA YAFUNGUA FURSA ZA AJIRA KWA VIJANA

Na: OWM (KAM) - Dar es Salaam

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Sangu amesema Maonesho ya Ajira kati ya Tanzania na China yameendelea kufungua fursa mbalimbali za ajira kwa vijana wa Kitanzania kupitia uwekezaji, uhamishaji wa teknolojia na kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi zinazotekelezwa na kampuni za China nchini.

Mhe. Sangu amesema hayo leo Juni 16, 2026 wakati akizindua Maonesho ya Ajira ya Tano (5) kati ya Tanzania na China yaliyofanyika katika viwanja vya Maktaba ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Amesema kuwa kupitia maonesho hayo ya ajira, vijana wa Kitanzania wameunganishwa na waajiri, wameanzisha kazi zenye mafanikio na kupata uzoefu muhimu kupitia fursa zilizoundwa na jukwaa hilo.

Vilevile, amesema makampuni ya Kichina yanayofanya kazi nchini Tanzania yamekuwa washirika muhimu kupitia uwekezaji katika miundombinu, viwanda, sekta ya madini, teknolojia ya habari, usafirishaji, nishati na sekta nyingine za kimkakati.

Ameongeza kuwa, Makampuni hayo yamechangia kwa kiasi kikubwa katika ukuaji wa uchumi na kutoa fursa za ajira kwa Watanzania.

Kadhalika, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kutoa fursa za ajira zenye tija kwa wananchi na suala hilo limekuwa kipaumbele cha kitaifa.

Amesema, Serikali inatekeleza sera na programu zinazohamasisha viwanda, mafunzo ya ujuzi, ujasiriamali, ufanisi wa soko la ajira na kazi zenye staha kwa wote.

Pia, amesema kupitia Dira ya Tanzania 2050, imewekwa wazi kuwa kila kijana nchini anapaswa kupata nafasi ya kujipatia ujuzi, kupata ajira yenye staha na kushiriki kikamilifu katika mabadiliko ya kiuchumi ya Taifa.

“Tanzania ni Taifa lenye vijana wengi, wameelimika, wana ndoto, wabunifu na wako tayari kuchangia katika maendeleo ya taifa,” amesema Waziri Sangu.

Kwa upande mwingine, Mhe. Sangu amesema Serikali ya Tanzania itaendelea kuimarisha ushirikiano na Serikali ya China katika uhamishaji wa ujuzi, teknolojia, ubunifu na utaalamu ili kuongeza ushindani wa taifa katika uchumi wa dunia unaobadilika kwa kasi.

Naye, Balozi wa China nchini Tanzania, Mheshimiwa Chen Mingjian, amesema Maonesho ya Ajira yaliyoandaliwa na Chama cha Makampuni ya China yanayofanya shughuli nchini Tanzania yamekuwa jukwaa muhimu kwa makampuni hayo na wahitimu wa Kitanzania kukutana na kujadili kwa pamoja kuhusu fursa za ajira.

Aidha, amezitaka kampuni hizo kuendelea kuwa daraja la ushirikiano kwa kutoa nafasi zaidi za ajira kwa Watanzania.

Zaidi ya kampuni 60 zinashiriki katika maonesho hayo kutoka sekta mbalimbali ikiwemo Uhandisi, Viwanda, Biashara, Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, Fedha pamoja na Huduma.

Maonesho ya Ajira ya Tano (5) kati ya China na Tanzania yamelenga kutangaza na kuwaunganisha vijana wahitimu na wenye ujuzi wa Kitanzania na makampuni ya Kichina, ili kuimarisha ajira, ubunifu na ushirikiano wa kiuchumi kwa manufaa ya pande zote mbili.

Post a Comment

0 Comments