

Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Mhe. Emmanuel Cherehani, akizungumza na wananchi wakati wa kukagua eneo la ujenzi wa Shule ya Sekondari Kalo kabla ya kukabidhi Sh. milioni 603.8 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.

Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Mhe. Emmanuel Cherehani, akizungumza na wananchi wakati wa kukagua eneo la ujenzi wa Shule ya Sekondari Kalo kabla ya kukabidhi Sh. milioni 603.8 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.
Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Ushetu, Emmanuel Malima, akieleza hatua za utekelezaji wa ujenzi wa Shule ya Sekondari Kalo baada ya kupokelewa kwa fedha za Sh. milioni 603.8.
Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Mhe. Emmanuel Cherehani (katikati), akitembelea na kukagua eneo la ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari Isanga katika Kata ya Idahina, Julai 20, 2026, ili kujionea maendeleo ya utekelezaji wa mradi unaofadhiliwa na Serikali ya Awamu ya Sita kwa zaidi ya Shilingi milioni 603.
Na Kadama Malunde – Malunde 1 Blog
Ndani ya siku mbili mfululizo, Jimbo la Ushetu limeandika sura mpya katika historia ya maendeleo ya elimu baada ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kutoa zaidi ya shilingi bilioni 1.2 kwa ajili ya ujenzi wa shule mbili mpya za sekondari katika Kata za Ulewe na Idahina.
Fedha hizo ambazo ni zaidi ya shilingi milioni 603.8 kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Sekondari Kalo katika Kata ya Ulewe na zaidi ya shilingi milioni 603.8 kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Sekondari Isanga katika Kata ya Idahina, zimekuja kuwa majibu ya muda mrefu ya wananchi waliokuwa wakihitaji huduma ya elimu kusogezwa karibu na makazi yao.
Mbele ya wananchi wake, Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Mhe. Emmanuel Cherehani, amekuwa mstari wa mbele kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo, akihakikisha fedha za maendeleo zinazotolewa na Serikali zinawafikia wananchi na kutekeleza malengo yaliyokusudiwa.
KALO: AHADI YATIMIA, MILANGO YA ELIMU YAFUNGULIWA ULEWE
Katika Kata ya Ulewe, wananchi wamepokea kwa furaha ujio wa fedha za shilingi milioni 603.8 kwa ajili ya ujenzi wa Shule ya Sekondari Kalo, mradi unaotarajiwa kubadilisha mazingira ya upatikanaji wa elimu kwa vijana wa eneo hilo.
Akikagua eneo la ujenzi na kukabidhi fedha hizo, Mhe. Cherehani amesema hatua hiyo ni utekelezaji wa ahadi yake kwa wananchi waliokuwa wamewasilisha maombi ya ujenzi wa shule hiyo.
"Hapa mliomba shule ya sekondari, mkaandaa maombi na muhtasari, nami nikawaahidi kuwa nitawaunga mkono. Leo nimetimiza ahadi hiyo kwa kuwaletea shilingi milioni 603.8 zilizotolewa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya ujenzi wa shule hii," amesema Cherehani.

Mbunge huyo amesisitiza kuwa fedha hizo zinapaswa kutumika kwa uadilifu ili kuhakikisha jamii inapata shule yenye ubora na mazingira rafiki kwa wanafunzi na walimu.
Kwa mujibu wa Afisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Ushetu, Emmanuel Malima, fedha hizo zitatumika kujenga miundombinu mbalimbali ikiwemo madarasa nane, jengo la utawala, vyumba vitatu vya maabara, maktaba, chumba cha kompyuta pamoja na matundu 16 ya vyoo.
Hatua hiyo inaashiria mwanzo wa safari mpya kwa watoto wa Ulewe ambao hapo awali walikuwa wakikabiliwa na changamoto ya kusafiri umbali mrefu kutafuta elimu ya sekondari.
ISANGA: SHULE MPYA YA SEKONDARI KUONDOA MSONGAMANO IDAHINA
Katika Kata ya Idahina, wananchi wa Kijiji cha Isanga nao wamepokea uwekezaji mkubwa wa elimu baada ya Serikali kutoa zaidi ya shilingi milioni 603 kwa ajili ya ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari Isanga.
Shule hiyo inatarajiwa kuwa mkombozi kwa wanafunzi wa Kata ya Idahina kwa kupunguza msongamano katika Shule ya Sekondari Idahina na kuongeza nafasi kwa vijana wengi zaidi kupata elimu katika mazingira bora.
Akizungumza wakati wa kukagua eneo la mradi huo, Mhe. Cherehani amesema fedha hizo zinatosha kuanza utekelezaji wa ujenzi na kwamba wananchi hawapaswi kubebeshwa mzigo wa michango.
"Nimewaletea shilingi milioni 603 kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ya Sekondari Isanga. Hakuna mwananchi atakayeombwa fedha. Namshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutupa fedha hizi za maendeleo," amesema.
Mbunge huyo amewataka wasimamizi wa mradi kuhakikisha kila shilingi inatumika kwa malengo yaliyokusudiwa ili shule hiyo ikamilike kwa ubora na kuanza kutoa huduma kwa wananchi.
CHEREHANI NA DIRA YA ELIMU YA USHETU
Ujenzi wa Shule za Sekondari Kalo na Isanga unaonyesha namna Serikali na viongozi wa eneo wanavyoweka nguvu katika kuboresha sekta ya elimu, ambayo ni msingi wa kujenga rasilimali watu yenye uwezo wa kuchangia maendeleo ya taifa.
Kwa Ushetu, miradi hiyo miwili si majengo pekee, bali ni uwekezaji katika ndoto za maelfu ya vijana wanaotamani kupata elimu bora bila vikwazo vya umbali.
Juhudi za Mbunge Emmanuel Cherehani katika kusimamia upatikanaji wa fedha hizo zimeongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, huku wananchi wakianza kuona matokeo ya uwekezaji wa Serikali katika maeneo yao.
Diwani wa Kata ya Ulewe, Mhe. Kulwa Emmanuel, amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kupeleka fedha za maendeleo katika maeneo ya vijijini, huku akimpongeza Mbunge Cherehani kwa kusimamia kwa karibu upatikanaji wa miradi hiyo.
Naye Diwani wa Kata ya Idahina, Mhe. Mathias Makashi, amesema ujenzi wa Shule ya Sekondari Isanga utakuwa suluhisho kubwa kwa changamoto ya msongamano wa wanafunzi na kuongeza fursa za elimu kwa vijana.
UWEKEZAJI UNAOTAZAMA KESHO
Kwa ujumla, zaidi ya shilingi bilioni 1.2 zinazowekezwa katika ujenzi wa shule mbili mpya za sekondari Ushetu ni hatua kubwa kuelekea kujenga kizazi chenye elimu na ujuzi.
Kalo na Isanga sasa zinakuwa alama ya mabadiliko katika sekta ya elimu ndani ya Ushetu, huku Mhe. Emmanuel Cherehani akiendelea kusisitiza matumizi sahihi ya fedha, usimamizi wa miradi na kuhakikisha wananchi wanapata thamani ya kila shilingi inayowekezwa.
Hatua hiyo inaendelea kuimarisha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kusogeza huduma za elimu karibu na wananchi na kuhakikisha mtoto wa Tanzania anapata nafasi sawa ya kujifunza na kufikia ndoto zake.





0 Comments