Ticker

6/recent/ticker-posts

MEDINOVA YAZINDUA HUDUMA YA TIBAMAZOEZI, YAIMARISHA HUDUMA ZA KIBINGWA

Na Mwandishi Wetu

Hospitali ya Medinova Specialized Polyclinic imezindua rasmi huduma ya Tibamazoezi (Physiotherapy) ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kupanua huduma za kibingwa na kuboresha upatikanaji wa huduma bora za afya nchini.

Uzinduzi huo unaenda sambamba na mpango wa hospitali hiyo wa kuongeza huduma mbalimbali za kibingwa, zikiwemo vyumba vya upasuaji (Operation Theatre), huduma za dharura na uangalizi maalumu (ICU), ili kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya wananchi.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo leo Julai 30, 2026 Jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa Tiba wa Medinova Specialized Polyclinic, Dkt. Imran Asif Bwaja, amesema hospitali hiyo imepiga hatua kubwa tangu ilipoanzishwa takribani miaka mitatu iliyopita na sasa inaingia katika awamu mpya ya upanuzi wa huduma za afya.

Amesema mafanikio hayo yamechangiwa na mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyowekwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, huku akiishukuru pia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam pamoja na viongozi wa Wilaya kwa ushirikiano wanaoendelea kuipatia hospitali hiyo.

Kwa upande wake, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ndani, Dkt. Selestine Mpiri, amesema tibamazoezi ni tiba ya utengamao inayotumia mazoezi maalumu na mbinu za kitaalamu kurejesha uwezo wa mwili bila matumizi ya dawa.

Amefafanua kuwa bado wananchi wengi wana dhana potofu kuhusu huduma hiyo kwa kuifananisha na massage, wakati tibamazoezi hulenga kubaini chanzo cha tatizo na kukitibu kwa njia za kitaalamu ili kuleta nafuu ya kudumu.

"Tibamazoezi hutumia mbinu mbalimbali ikiwemo mazoezi maalumu, tiba kwa kutumia mikono (Manual Therapy) na matumizi ya vifaa vya kisasa vya umeme (Electrotherapy) kulingana na mahitaji ya mgonjwa," amesema.

Dkt. Mpiri amesema huduma hiyo haimhusu mgonjwa aliyepata ajali au aliyefanyiwa upasuaji pekee, bali pia huwasaidia watu wenye matatizo ya mfumo wa upumuaji, mfumo wa fahamu, kizunguzungu, pamoja na wanawake wanaohitaji kuimarisha misuli ya nyonga kwa ajili ya kudhibiti mkojo na kupunguza maambukizi ya mara kwa mara ya njia ya mkojo.

Amewataka wananchi kuepuka kuiga mazoezi ya tibamazoezi wanayoyaona kwenye mitandao ya kijamii bila ushauri wa mtaalamu, akisisitiza kuwa kila mgonjwa hupangiwa mpango wa matibabu kulingana na umri, jinsia, historia ya afya na hali yake.

Aidha, amesema tibamazoezi si tiba yenye maumivu makali kama inavyodhaniwa na baadhi ya watu, bali huhitaji uvumilivu na kufuata ratiba ya matibabu ili kuuwezesha mwili na mfumo wa fahamu kurejesha uwezo wake wa kawaida.

Naye Mtaalamu wa Tibamazoezi wa Medinova Specialized Polyclinic, PT Witney Lema, amesema idara hiyo imeanzishwa ili kutoa huduma za utengamao bila matumizi ya dawa za kumeza wala sindano, kwa kutumia mbinu za kisasa zinazotambuliwa kimataifa.

Ametaja baadhi ya matatizo yanayotibiwa kuwa ni maumivu ya mgongo, shingo na magoti, matatizo ya misuli na mifupa, madhara ya ajali na kuvunjika mifupa, pamoja na matatizo ya mfumo wa fahamu ikiwemo wagonjwa waliopata kiharusi.

PT Lema amesema mahitaji ya huduma za tibamazoezi yanaendelea kuongezeka duniani kutokana na ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza, majeraha na changamoto nyingine zinazopunguza uwezo wa watu kufanya shughuli zao za kila siku.

"Idara hii imekuja kama suluhisho la kuwasaidia wananchi kurejesha uwezo wao wa kufanya kazi kwa ufanisi na kuboresha ubora wa maisha bila kutegemea matumizi makubwa ya dawa," amesema.

Ameeleza kuwa huduma hizo hutolewa kupitia njia kuu mbili ambazo ni Manual Therapy, ambapo mtaalamu hutumia mikono kutoa matibabu, na Electrotherapy inayotumia vifaa maalumu vya kisasa kusaidia kuharakisha mchakato wa tiba.

Mbali na huduma za tibamazoezi, Medinova Specialized Polyclinic pia hutoa huduma za kibingwa za magonjwa ya ndani, watoto, afya ya wanawake, magonjwa ya ngozi na urembo, afya ya kinywa na meno kupitia madaktari bingwa mbalimbali, sambamba na huduma za maabara ya kisasa inayotoa majibu kwa haraka na kwa usahihi.

Post a Comment

0 Comments