Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Mahusiano ya kidiplomasia kati ya Ufalme wa Morocco na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yameendelea kuimarika kwa kasi tangu ziara ya kihistoria ya Kiserikali ya Mfalme Mtukufu Mohammed VI nchini Tanzania mwaka 2016, huku ushirikiano katika sekta mbalimbali ukizidi kupanuka na kuleta manufaa kwa mataifa yote mawili.
Hayo yalisemwa jijini Dar es Salaam na Balozi wa Ufalme wa Morocco nchini Tanzania, Zakaria El Goumiri, wakati wa maadhimisho ya miaka 27 tangu kutawazwa kwa Mfalme Mtukufu Mohammed VI, tukio linaloashiria karibu miongo mitatu ya uongozi ulioleta mageuzi ya kitaifa na maendeleo endelevu nchini Morocco.
Balozi El Goumiri alisema tangu ziara ya Mfalme Mohammed VI mwaka 2016, ushirikiano wa pande mbili umeongezeka kwa kiwango kikubwa katika sekta za kilimo, biashara, benki, elimu, uwekezaji, bima na utamaduni, jambo linaloonyesha dhamira ya mataifa hayo kuimarisha ushirikiano wa Kiafrika unaojengwa katika misingi ya kuheshimiana, mshikamano na maendeleo endelevu.
Alieleza kuwa uhusiano huo umeendelea kuwa mfano wa ushirikiano wa kimkakati barani Afrika, huku nchi hizo zikitumia fursa zilizopo kukuza biashara, uwekezaji na kubadilishana uzoefu katika nyanja mbalimbali za maendeleo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Ngwaru Jumanne Maghembe, alisema Tanzania inaithamini Morocco kama mshirika muhimu wa maendeleo na imeendelea kushuhudia matokeo chanya ya ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.
Dkt. Maghembe aliiomba Morocco kuongeza ushirikiano zaidi katika sekta za uchumi, hususan biashara, uwekezaji, viwanda na miradi ya maendeleo, ili wananchi wa mataifa yote mawili wanufaike zaidi na fursa zinazotokana na uhusiano huo.
Alisema Serikali ya Tanzania inaendelea kuhamasisha ushirikiano wa karibu na mataifa ya Afrika kupitia biashara na uwekezaji, akisisitiza kuwa ushirikiano wa Tanzania na Morocco una nafasi kubwa ya kuchochea ukuaji wa uchumi na kuimarisha ustawi wa wananchi wa pande zote mbili.
Maadhimisho ya miaka 27 ya kutawazwa kwa Mfalme Mohammed VI yamekuwa pia fursa ya kutathmini mafanikio ya Morocco katika kipindi cha uongozi wake, pamoja na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia na washirika wake wa kimataifa, ikiwemo Tanzania.











0 Comments