NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
MAMLAKA ya Elimu Tanzania (TEA) imeeleza kuwa imejikita katika kutafuta rasilimali zitakazowezesha utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2023, kwa kuwekeza nguvu katika maeneo matatu ya kipaumbele ambayo ni ujenzi wa miundombinu kwa elimu ya lazima ya miaka 10, maendeleo ya mkondo wa amali pamoja na matumizi ya nishati safi na uhifadhi wa mazingira shuleni.
Akizungumza leo Julai 6, 2026 atika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba), Meneja wa Utafutaji wa Rasilimali na Hamasa wa TEA, Dkt. George Mwafulu, amesema taasisi hiyo inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi kuhakikisha sekta ya elimu inapata rasilimali za kutosha kukidhi mahitaji yanayoongezeka kutokana na utekelezaji wa sera mpya ya elimu.
Amesema eneo la kwanza la kipaumbele linahusu upatikanaji wa rasilimali kwa ajili ya miradi itakayowezesha utekelezaji wa elimu ya lazima ya miaka 10, ambapo kuanzia Januari 2028 kunatarajiwa kuwa na ongezeko kubwa la wanafunzi watakaojiunga na kidato cha kwanza.
"Kutokana na utekelezaji wa sera mpya ya elimu, wanafunzi wa mikondo ya darasa la sita na darasa la saba wataingia kidato cha kwanza kwa wakati mmoja. Hii inamaanisha kuwa zaidi ya wanafunzi milioni tatu wanatarajiwa kujiunga na elimu ya sekondari, hali inayoongeza mahitaji makubwa ya madarasa, mabweni, samani, vifaa vya kujifunzia na miundombinu mingine muhimu," amesema Dkt. Mwafulu.
Amefafanua kuwa TEA inalenga kuhakikisha inapata rasilimali zitakazosaidia kujenga mazingira bora ya kufundishia na kujifunzia ili kukidhi ongezeko hilo la wanafunzi.
Dkt. Mwafulu amesema eneo la pili la kipaumbele ni utekelezaji wa mkondo wa amali, ambao umeanzishwa chini ya sera mpya ya elimu kwa lengo la kuwajengea wanafunzi ujuzi wa vitendo unaoendana na mahitaji ya soko la ajira.
Amesema mkondo huo unahitaji uwekezaji mkubwa katika miundombinu maalumu, karakana, maabara pamoja na vifaa vya kisasa vya kufundishia ili wanafunzi waweze kupata elimu yenye kuzingatia mafunzo kwa vitendo.
"Mahitaji ya mkondo wa amali ni mapya na makubwa. Ndiyo maana tunaendelea kutafuta ushirikiano wa wadau mbalimbali ili kusaidia upatikanaji wa vifaa na miundombinu itakayowezesha utekelezaji wake kwa ufanisi," ameeleza.
Aidha, amesema eneo la tatu la kipaumbele ni mazingira na matumizi ya nishati safi mashuleni, hususan katika shule zinazotekeleza programu za upishi kwa wanafunzi.
Amesema TEA inatafuta rasilimali zitakazosaidia matumizi ya teknolojia za nishati safi, hatua itakayochangia kupunguza uharibifu wa mazingira, kuboresha mazingira ya shule na kuhakikisha matumizi endelevu ya rasilimali kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Katika kutekeleza mikakati hiyo, Dkt. Mwafulu amesema TEA inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kwa mujibu wa sheria, wakiwemo washirika wa maendeleo, sekta binafsi, taasisi za umma na wadau wengine wa elimu.
Ametaja baadhi ya wadau ambao tayari wanashirikiana na TEA kuwa ni UNICEF katika utekelezaji wa miradi ya elimu pamoja na kampuni ya Halotel, ambayo imeingia makubaliano ya ushirikiano na mamlaka hiyo.
Dkt. Mwafulu ametoa wito kwa wadau wengine kuendelea kushirikiana na TEA kwa kuchangia rasilimali na utaalamu ili kuimarisha sekta ya elimu na kuhakikisha utekelezaji wa sera mpya unaleta matokeo yaliyokusudiwa kwa maendeleo ya taifa.
TEA ni taasisi ya umma inayosimamia Mfuko wa Elimu wa Taifa ambao una jukumu la kutafuta raslimali fedha na vifaa kisha kuvielekeza kwenye uboreshaji wa miundombinu ya elimu nchini ikiwa pamoja na ujenzi wa nyumba za walimu, madarasa, maabara za sayansi, maabara za TEHAMA na vyoo.








0 Comments