NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) imepongezwa kwa kukamilisha kwa wakati uandishi na uchapaji wa vitabu vya Elimu ya Dini ya Kiislamu (EDK) kwa Kidato cha Sita, hatua inayowezesha wanafunzi kuanza kutumia vitabu hivyo katika utekelezaji wa mtaala mpya wa elimu.
Pongezi hizo zimetolewa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, wakati alipokabidhi vitabu hivyo kwa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) na Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar katika hafla iliyofanyika Julai 22, 2026, kwenye Ukumbi wa Mfalme Mohammed wa Sita, Makao Makuu ya BAKWATA jijini Dar es Salaam.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi wa dini, maafisa wa Serikali na wadau mbalimbali wa sekta ya elimu na dini ya Kiislamu.
Akizungumza katika hafla hiyo, Prof. Mkenda alisema Serikali itaendelea kutekeleza Sera ya Elimu kwa kuhakikisha kila mwanafunzi nchini anapata elimu yenye ubora na fursa sawa za kujifunza, bila kujali eneo analotoka au somo analolisoma.
Alisema kukamilika kwa vitabu hivyo ni sehemu ya utekelezaji wa maboresho ya Sera ya Elimu na Mitaala ya mwaka 2023, ambapo wadau mbalimbali walipendekeza kuimarishwa kwa ufundishaji wa somo la Elimu ya Dini ya Kiislamu katika shule.
Prof. Mkenda aliishukuru BAKWATA kwa ushirikiano wake katika kufanikisha mchakato huo, akieleza kuwa kupitia Mufti Mkuu wa Tanzania, taasisi hiyo ilisaidia kuanzishwa kwa Taasisi ya Kusimamia Ufundishaji wa Dini ya Kiislamu Shuleni (TISTA), ambayo itasimamia utekelezaji wa somo hilo.
"Mchakato huu umefanywa kwa karibu sana na Waislamu wote. Tulipata baraka za Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na ushirikiano wa Mufti Mkuu na wadau wote wa dini ya Kiislamu," alisema Prof. Mkenda.
Aliongeza kuwa kupitia TISTA chini ya BAKWATA, wanafunzi watapata mazingira bora ya kujifunza somo la Elimu ya Dini ya Kiislamu kwa kuzingatia viwango vya kitaaluma vilivyowekwa.
Waziri huyo pia aliipongeza TET chini ya uongozi wa Mkurugenzi Mkuu, Dkt. Aneth Komba, kwa kuhakikisha uandishi, uhakiki na uchapaji wa vitabu hivyo unakamilika kwa wakati, hatua ambayo amesema itawawezesha wanafunzi kuanza kuvitumia mara moja shuleni.
"Nina imani vitabu hivi vitatumika kama ilivyokusudiwa na vitasaidia kuongeza ubora wa ufundishaji na ujifunzaji wa somo la Elimu ya Dini ya Kiislamu kwa wanafunzi wa Kidato cha Sita," alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa TISTA, Bw. Musa Kundecha, alisema upatikanaji wa vitabu hivyo ni hatua muhimu katika kuboresha ufundishaji na ujifunzaji wa somo hilo, akieleza kuwa vitawawezesha walimu na wanafunzi kuwa na rejea sahihi zinazokidhi mahitaji ya mtaala.
Naye mwakilishi wa Mufti Mkuu wa Tanzania, Naibu Kadhi, Bw. Ali Ngeruko, alisema kukabidhiwa kwa vitabu hivyo ni hatua kubwa katika kuimarisha elimu ya dini kwa wanafunzi na kutimiza ahadi ya Serikali ya kuhakikisha vifaa vya kujifunzia vinapatikana kwa wakati.
Aliishukuru Serikali kwa kushirikisha wadau wa dini katika mchakato mzima wa maandalizi ya vitabu hivyo na kueleza kuwa ushirikiano huo umejenga msingi imara wa kuendeleza elimu ya dini katika shule.
Vitabu vya Elimu ya Dini ya Kiislamu kwa Kidato cha Sita vitasambazwa katika shule zote za Tanzania Bara na Zanzibar zinazofundisha somo hilo ili kuhakikisha wanafunzi wanapata vitendea kazi vinavyowawezesha kujifunza kwa ufanisi.
0 Comments