Jamii, kampuni binafsi na wadau mbalimbali wametakiwa kuongeza juhudi za kusaidia wanafunzi wenye mahitaji maalum kwa kuwapatia huduma za afya, vifaa saidizi na mahitaji ya kielimu ili kuwawezesha kupata elimu bora na kutimiza ndoto zao.
Wito huo umetolewa na Elvis Lyimo, Mkuu wa Idara ya Elimu Maalum katika Shule ya Sekondari Pugu, wakati ALC Group, wauzaji wa vilainishi vya Flying Horse Lubricant, ilipofika shuleni hapo na kutoa msaada kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Kupitia msaada huo, wanafunzi 50 wamepatiwa bima ya afya, huku baadhi yao wakipatiwa viti mwendo pamoja na kompyuta kwa ajili ya kuwawezesha kushiriki vizuri zaidi katika masomo na shughuli zao za kila siku.
Lyimo amesema msaada huo una umuhimu mkubwa kwa wanafunzi wenye ulemavu, hususan wale wanaotoka katika familia zenye uwezo mdogo kiuchumi na ambao mara nyingi hukabiliwa na changamoto ya kupata huduma za afya na vifaa muhimu vya kuwasaidia katika ujifunzaji.
“Msaada huu utawasaidia wanafunzi wenye ulemavu wa viungo na changamoto ya kuandika, ambao wengi wao wanatoka katika familia zenye hali duni kiuchumi,” amesema Lyimo.
Amesema baadhi ya wanafunzi wenye mahitaji maalum hukabiliwa na changamoto za kupata viti mwendo, magongo ya kutembelea, magodoro, vifaa vya kujifunzia na mahitaji mengine muhimu, huku gharama za matibabu zikiwa changamoto kwa familia nyingi.
Kwa mujibu wa Lyimo, Shule ya Sekondari Pugu ina jumla ya wanafunzi 85 wenye mahitaji maalum, hali inayofanya mahitaji ya huduma na vifaa kuwa makubwa zaidi licha ya Serikali kuendelea kutoa huduma mbalimbali.
Amesema ushiriki wa wadau zaidi ni muhimu katika kuziba pengo lililopo na kuhakikisha wanafunzi hao wanapata fursa sawa ya elimu na maendeleo.
WAZAZI WATAKIWA KUTOWAFICHA WATOTO WENYE ULEMAVU
Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari Pugu, Patrick Sinyinza, amewataka wazazi na walezi kutowaficha watoto wenye ulemavu majumbani, bali kuwapeleka shuleni ili wapate elimu na fursa ya kuendeleza vipaji na uwezo wao.
Sinyinza amesema watoto wenye mahitaji maalum wana uwezo mkubwa wa kufanya vizuri kitaaluma iwapo watapewa mazingira rafiki, msaada na fursa zinazostahili.
Amesema msaada uliotolewa na ALC Group umefika wakati muafaka kwa kuwa wanafunzi wenye ulemavu wanahitaji huduma za afya mara kwa mara pamoja na vifaa vinavyowawezesha kushiriki kikamilifu katika masomo.
“Wazazi wasiwanyime watoto wenye ulemavu haki yao ya kupata elimu kwa kuwaficha nyumbani. Watoto hawa wana uwezo mkubwa wa kufanya vizuri kitaaluma,” amesema Sinyinza.
Ameeleza kuwa Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kuboresha miundombinu na mazingira ya shule ili kuwawezesha wanafunzi wenye na wasio na ulemavu kusoma pamoja katika mazingira yanayozingatia mahitaji yao.
Shule ya Sekondari Pugu ina jumla ya wanafunzi 989 na walimu 74, ambapo walimu 26 wamepatiwa mafunzo maalum ya elimu ili kuwawezesha kuwahudumia wanafunzi wenye mahitaji maalum.
MWANAFUNZI MWENYE MAHITAJI MAALUM APATA ALAMA SABA
Sinyinza amesema mafanikio ya wanafunzi wenye mahitaji maalum katika shule hiyo ni ushahidi kuwa ulemavu si kikwazo cha kufikia mafanikio ikiwa mwanafunzi atapatiwa msaada unaostahili.
Ametoa mfano wa mwanafunzi wa Kidato cha Sita aliyefanya mtihani mwaka huu na kupata alama saba na Daraja la Kwanza, akisema mafanikio hayo yanaonyesha uwezo mkubwa walionao wanafunzi wenye mahitaji maalum.
“Hii inaonyesha uwezo mkubwa walionao watoto hawa. Wapo wanafunzi wasio na ulemavu ambao hawakupata alama saba, lakini mwanafunzi mwenye mahitaji maalum ameweza kufanya hivyo. Wanachohitaji ni msaada na fursa,” amesema.
ALC GROUP YAAHIDI KUENDELEA KUSAIDIA
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya msaada huo, Emmanuel Shija, Balozi wa ALC Group, wauzaji wa vilainishi vya Flying Horse Lubricant, ambaye pia ni Bingwa wa WBC Muay-Thai Tanzania, amesema mchango huo ni sehemu ya utekelezaji wa wajibu wa kampuni kwa jamii.
Shija amesema kampuni imeamua kuanza na wanafunzi 50 kwa kuwapatia bima za afya, viti mwendo na kompyuta, huku ikiweka mkakati wa kuendelea kusaidia wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Amesema watu wenye ulemavu na wanaoishi katika mazingira magumu mara nyingi husahaulika katika jamii, hivyo ALC Group imeona umuhimu wa kutumia sehemu ya mafanikio yake kusaidia kuboresha maisha ya kundi hilo.
“Watu ambao wana changamoto au wanaoishi katika mazingira magumu mara nyingi husahaulika na jamii. Tumeamua kuanza na wanafunzi 50 kwa kuwapatia bima za afya, viti mwendo na kompyuta kwa sababu tunaamini ni muhimu kuwakumbuka na kuwasaidia wanaohitaji msaada,” amesema Shija.
Amesema ALC Group itaendelea kugharamia bima za afya kwa baadhi ya wanafunzi wenye mahitaji maalum ili kuwawezesha kupata matibabu kwa wakati na kupunguza mzigo wa gharama kwa familia zao.
Aidha, amesema kampuni hiyo itaendelea kutoa vifaa vya usafiri kwa baadhi ya wanafunzi, ikiwemo baiskeli za magurudumu matatu, ili kuwawezesha wanafunzi wenye changamoto za ulemavu wa viungo kusafiri kwa urahisi na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kila siku.
Shija amesema lengo la kampuni si kutoa msaada wa mara moja pekee, bali kujenga utamaduni endelevu wa kuirudishia jamii sehemu ya mafanikio yanayopatikana kupitia shughuli za kampuni.
“Lengo letu si kutoa msaada wa mara moja, bali kujenga utamaduni wa kutoa na kuirudishia jamii sehemu ya mafanikio tunayoyapata. Tunaamini kila taasisi ina nafasi ya kuleta mabadiliko chanya katika maisha ya watu wenye mahitaji maalum,” amesema.
WANAFUNZI WASHUKURU MSAADA
Kwa upande wa wanafunzi, Thobias Masumbulko, aliyewakilisha wanafunzi wenzake, ameishukuru ALC Group kwa msaada huo na kusema vifaa vilivyotolewa vina umuhimu mkubwa katika maisha yao.
Amesema wakati mwingine watu wanaweza kuona msaada kama huo kuwa ni mdogo, lakini kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum una thamani kubwa kwa sababu unawapatia vitu ambavyo hapo awali walikosa.
“Tunawashukuru kwa kile mlichotupatia. Mnaweza kufikiri ni kidogo, lakini kwetu ni kitu kikubwa kwa sababu ni vitu ambavyo hatukuwa navyo kabla,” amesema.
Masumbulko amewataka wazazi na jamii kwa ujumla kutowatenga watoto wenye ulemavu, akisisitiza kuwa wana uwezo wa kufanya mambo makubwa iwapo watapewa fursa na msaada unaostahili.
Ameeleza pia kuwa walimu wa shule hiyo wamekuwa na mchango mkubwa katika kuwajengea wanafunzi wenye mahitaji maalum kujiamini na kuwahamasisha kuangalia uwezo wao badala ya kujikita katika changamoto zao.










0 Comments