Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imezindua rasmi Kielelezo cha Faida Rejea ya Dhamana za Serikali (Tanzania Sovereign Yield Curve), hatua inayotarajiwa kuongeza uwazi, ushindani na ufanisi katika soko la Dhamana za Serikali na kuimarisha mazingira ya uwekezaji nchini.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo uliofanyika katika makao makuu ya BoT jijini Dar es Salaam, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba, alisema kielelezo hicho kimetokana na miamala halisi ya soko la upili na kitawawezesha wawekezaji kufuatilia mwenendo wa viwango vya faida pamoja na kufanya maamuzi sahihi ya uwekezaji.
Alisema pia kielelezo hicho kitakuwa rejea muhimu katika kupanga bei za mikopo, mikopo ya nyumba na hatifungani za kampuni kwa kutumia viwango rejea visivyo na hatari (risk-free benchmark rates), hatua itakayoongeza ufanisi katika sekta ya fedha.
Gavana Tutuba alieleza kuwa matumizi ya kielelezo hicho yataongeza imani ya wawekezaji wa ndani na nje, kuvutia mitaji ya kigeni na kuongeza ushindani katika soko la dhamana za Serikali.
Aidha, alisisitiza kuwa soko la dhamana lina mchango mkubwa katika kuiwezesha Serikali kupata rasilimali za kugharamia miradi ya maendeleo, hivyo kuendelea kuchochea utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Kwa upande wake, Kamishna wa Idara ya Usimamizi wa Madeni wa Wizara ya Fedha, Bw. Japhet Justine, alisema uzinduzi wa kielelezo hicho ni hatua ya kihistoria katika kuimarisha soko la Dhamana za Serikali na kujenga miundombinu ya masoko inayokidhi viwango vya kimataifa.
Alifafanua kuwa kielelezo hicho kinatatua changamoto ya muda mrefu ya ukosefu wa taarifa za kutosha kuhusu viwango halisi vya faida vinavyotokana na mauzo na manunuzi ya dhamana katika soko la upili, hali ambayo ilikuwa ikifanya kuwa vigumu kupanga bei sahihi za dhamana.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), CPA Nicodemas Mkama, Mkurugenzi Mtendaji wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Bw. Peter Nalitolela, viongozi na watumishi wa Wizara ya Fedha, wawakilishi wa Idara ya Hazina ya Marekani pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya fedha nchini.


















0 Comments