Mwanzilishi na Mwenyekiti wa Gender, Health and Sustainable Environment (GEHESE), Lilian Lihundi akizungumza wakati wa warsha ya uhamasishaji na kujenga uwezo kuhusu “Market Waste to Wealth” iliyofanyika Mbezi, Dar es Salaam
Shirika la GEHESE limeendesha warsha ya uhamasishaji na kujenga uwezo kuhusu “Market Waste to Wealth” ikiwa na lengo la kuhamasisha jamii kuhusu namna taka za sokoni zinavyoweza kusimamiwa, kuchakatwa na kubadilishwa kuwa rasilimali zenye thamani kiuchumi.
Akizungumza wakati wa warsha hiyo iliyofanyika Agosti 14, 2026, katika eneo la Mbezi, Dar es Salaam, Mwanzilishi na Mwenyekiti wa GEHESE, Lilian Lihundi amesema usimamizi mzuri wa taka unaweza kusaidia kulinda mazingira na kuongeza fursa za kiuchumi kwa jamii.
Ameeleza kuwa Taka zinazozalishwa katika masoko zinaweza kubadilishwa kuwa bidhaa zenye thamani na kuwa chanzo cha kipato.
Lihundi amesema taka za masokoni, hususan taka za kikaboni, zinaweza kuchakatwa na kuzalisha bidhaa mbalimbali zikiwemo mboji, chakula cha mifugo pamoja na bidhaa nyingine zenye thamani.
Amesema matumizi ya teknolojia mpya, ikiwemo Black Soldier Fly Larvae (BSFL), yanaweza kuongeza thamani ya taka za kikaboni na kufungua fursa zaidi za kiuchumi.
Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Mbezi, Pius Ragiro Nyantori, amesema elimu ya utenganishaji taka inapaswa kupewa kipaumbele katika masoko na jamii ili kuwezesha taka kutumika kama rasilimali.
Nyantori amesema Serikali itaweka mazingira yatakayowezesha kuanzishwa kwa vituo vya uchakataji taka katika masoko ya kata hiyo.
Amesema vituo hivyo vinaweza kuwa kichocheo cha ajira na biashara kwa vijana, wanawake na wafanyabiashara, kupitia shughuli za ukusanyaji, utenganishaji na uchakataji wa taka.
Naye Mratibu wa Programu ya Taka ni Mali wa GEHESE, Catherine Sembua, ametoa mafunzo kuhusu usimamizi wa taka, aina mbalimbali za taka na umuhimu wa kuzitenganisha tangu zinapozalishwa.
Sembua, ambaye pia ni mtafiti wa masuala ya usimamizi wa taka na mwanazuoni wa Shahada ya Uzamivu katika eneo hilo, amewataka wafanyabiashara wa masokoni kuanza kuziona taka kama fursa badala ya changamoto.
Amesema utenganishaji wa taka tangu zinapozalishwa ni muhimu katika kurahisisha uchakataji na kuongeza uwezekano wa taka hizo kubadilishwa kuwa bidhaa zenye thamani.
Sembua amesema Kituo cha Ubunifu cha GEHESE kitaendelea kuwajengea uwezo wafanyabiashara na jamii kuhusu utenganishaji wa taka na namna ya kuzibadili kuwa rasilimali kupitia dhana ya uchumi wa mzunguko (circular economy).
Amesema kupitia uchumi wa mzunguko, taka zinaweza kurejeshwa katika matumizi na hivyo kupunguza athari zake kwa mazingira huku zikitoa fursa za ajira, biashara na kipato kwa jamii.
Diwani wa Kata ya Mbezi, Pius Ragiro Nyantori, kizungumza wakati wa warsha ya uhamasishaji na kujenga uwezo kuhusu “Market Waste to Wealth” iliyofanyika Mbezi, Dar es Salaam
wanzilishi na Mwenyekiti wa Gender, Health and Sustainable Environment (GEHESE), Liliani Lihundi pamoja na Diwani wa Kata ya Mbezi, Pius Ragiro Nyantori, wakiteta jambo .





















0 Comments