Na: OWM – TAMISEMI, Mbeya
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM-TAMISEMI), Mhe. Prof. Riziki Shemdoe, amezitaka Halmashauri zote nchini kutumia michezo kama nyenzo ya kuimarisha afya, ustawi, mshikamano na tija kwa watumishi, ili kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.
Prof. Shemdoe ametoa wito huo Agosti 23, 2026 jijini Mbeya wakati akifungua rasmi Mashindano ya Michezo ya Watumishi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa Tanzania (SHIMISEMITA), kwa niaba ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba.
Akizungumza katika ufunguzi huo, Prof. Shemdoe amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuyarejesha tena mashindano ya SHIMISEMITA mwaka 2023 baada ya kusitishwa, akitambua kwamba michezo ni sehemu muhimu ya kujenga afya ya mwili na akili, kuimarisha mahusiano kazini na kukuza ushirikiano miongoni mwa watumishi kutoka Halmashauri mbalimbali nchini.
“Leo hii mmekutana watumishi zaidi ya 5,000 kutoka katika Halmashauri 177. Kila mmoja anao wajibu wa kujenga mahusiano mazuri na watumishi wa Halmashauri nyingine, kwani michezo ni afya, michezo ni kiunganishi. Hivyo, tumieni fursa hii kujenga afya zenu na kuimarisha ushirikiano miongoni mwenu,” amesema.
Aidha, Prof. Shemdoe amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha ushiriki wa michezo unawahusisha watumishi kutoka maeneo mbalimbali, badala ya watumishi wa Makao Makuu pekee.
Amesema watumishi kutoka ngazi za kata, vijiji na vitongoji wanapaswa kupewa fursa ya kushiriki, kwa kuwa michezo itawajengea ari na morali ya kutekeleza majukumu yao, ikiwemo ukusanyaji wa mapato, ikizingatiwa kuwa mtumishi mwenye afya njema ya mwili na akili atatekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kutoa huduma bora kwa wananchi.

Sanjari na hilo, Prof. Shemdoe amezitaka Halmashauri kuwaandaa na kuwajengea uwezo wananchi kutumia fursa zitakazotokana na Mashindano ya Soka kwa Timu za Taifa Barani Afrika (AFCON 2027). Amesema mashindano hayo si suala la michezo pekee, bali yatatoa fursa za kiuchumi, kijamii, kiutamaduni na hususan katika sekta ya utalii, ambayo ni miongoni mwa sekta muhimu katika kuiingizia Tanzania fedha za kigeni.
Kutokana na umuhimu wa michezo kwa afya na utendaji wa watumishi wa umma, Prof. Shemdoe amezitaka Halmashauri zote nchini kuhakikisha michezo ya SHIMISEMITA inawekewa kifungu katika bajeti zao na kutengewa fedha ili kuwawezesha watumishi kushiriki kikamilifu. Amesema uwekezaji katika michezo ni uwekezaji katika afya ya mwili na akili za watumishi, jambo litakalosaidia kuongeza morali, ufanisi na tija katika utekelezaji wa majukumu ya Serikali na utoaji wa huduma kwa wananchi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Beno Malisa, amemshukuru Prof. Shemdoe kwa Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI kuyaleta mashindano ya SHIMISEMITA mkoani Mbeya, na kuahidi kuwa uongozi wa mkoa umejipanga kuhakikisha usalama na ustawi wa wanamichezo wote wakati wa mashindano hayo. Aidha, Mhe. Malisa amemshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia mashindano ya SHIMISEMITA kuendelea kufanyika nchini.
Naye, Katibu Mkuu wa SHIMISEMITA, Bw. Henry Kapella, ameiomba Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, ikiwa mlezi wa SHIMISEMITA, kuendelea kuzihimiza Halmashauri kutenga bajeti kwa ajili ya kuwawezesha watumishi kushiriki mashindano hayo kila mwaka. Ameshauri pia TAMISEMI kuweka kigezo cha uwepo wa fedha zilizotengwa kwa ajili ya michezo ya SHIMISEMITA katika mchakato wa kupitisha bajeti za Halmashauri, ili kuhakikisha watumishi wanapata fursa endelevu ya kushiriki michezo.
Mashindano ya SHIMISEMITA mwaka huu yamebeba kaulimbiu “Tuko Tayari kwa AFCON 2027,” ikiwa ni ujumbe unaosisitiza utayari wa Tanzania kutumia fursa za michezo, kuimarisha afya na mshikamano wa watumishi, pamoja na kunufaika na fursa za kiuchumi, kijamii, kiutamaduni na kiutalii zitakazotokana na AFCON 2027.
















0 Comments