Ticker

6/recent/ticker-posts

PROF. NOMBO ATEMBELEA BANDA LA TUME YA TAIFA YA UNESCO TANGA





Na: Julitha Mlay
Tanga, 20 Agosti 2026

Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, leo Agosti 20, 2026 ametembelea Banda la Tume ya Taifa ya UNESCO ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika maadhimisho ya Wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu Kitaifa yanayoendelea jijini Tanga.

Katika ziara hiyo, Prof. Nombo amepata fursa ya kujionea shughuli na maudhui mbalimbali yanayotolewa na Tume katika kuelimisha umma kuhusu UNESCO, majukumu ya Tume na programu zake katika maeneo ya elimu, sayansi, utamaduni, mawasiliano na taarifa.

Prof. Nombo alikuwa ameambatana na Dkt. Fredrick Salukele, Mkurugenzi wa Elimu ya Ufundi, ambapo walipata fursa ya kufahamu zaidi namna Tume inavyotumia majukwaa ya kitaifa kuwafikia wananchi, wanafunzi, walimu, vijana na wadau wengine kwa taarifa kuhusu UNESCO na fursa zinazopatikana kupitia programu zake.

Ushiriki wa Tume katika Wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu Kitaifa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha elimu na uelewa wa umma kuhusu UNESCO, pamoja na kuonesha mchango wa elimu, sayansi, utamaduni, mawasiliano na taarifa katika kukuza maarifa, ubunifu na maendeleo endelevu nchini.

Kupitia jukwaa hilo, Tume inaendelea kuwasogezea wananchi taarifa kuhusu kazi za UNESCO na maeneo mbalimbali yanayohusiana na utekelezaji wa programu zake nchini Tanzania, huku ikihamasisha ushiriki wa jamii katika kutumia maarifa na fursa zilizopo kwa maendeleo ya mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Maadhimisho ya Wiki ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu Kitaifa yanaendelea jijini Tanga yakishirikisha taasisi na wadau mbalimbali wa sekta ya elimu, ujuzi na ubunifu kwa lengo la kuelimisha jamii kuhusu fursa, huduma na jitihada zinazochangia maendeleo ya rasilimali watu nchini.

Kwa habari zaidi kuhusu shughuli, programu, matukio na fursa mbalimbali za Tume ya Taifa ya UNESCO ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, endelea kutufuatilia kupitia kurasa zetu rasmi za mitandao ya kijamii:

Facebook na Instagram: @unesconatcomtz
Tume ya Taifa ya UNESCO — Kuelimisha, Kuhamasisha na Kushirikisha Jamii.

Post a Comment

0 Comments