Na Mwandishi Wetu
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan na Yoweri Museveni wa Uganda wameshuhudia utiaji saini wa Hati ya Makubaliano (MoU) ya kuendeleza ujenzi wa kiwanda cha kusafisha mafuta na Kitovu cha Nishati cha Kikanda Jijini Tanga, mradi unaotarajiwa kubadili taswira ya sekta ya nishati Afrika Mashariki.
Makubaliano hayo yaliyosainiwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Kampuni ya Taifa ya Mafuta ya Uganda (UNOC) na kampuni ya VTTO Bahrain, yanafungua njia kwa hatua za awali za kitaalamu na uwekezaji katika ujenzi wa miundombinu hiyo muhimu.
Akizungumza katika hafla hiyo,leo Ikulu jijini Dar es Salaam Waziri wa Nishati Deogratias Ndejembi alisema makubaliano hayo ni hatua muhimu katika kuimarisha ushirikiano wa Tanzania na Uganda kwenye sekta ya nishati.
Njejembi amesema kuwa mradi huo unatarajiwa kujumuisha kiwanda cha kusafisha mafuta, miundombinu ya kuhifadhi bidhaa za petroli, huduma za usafirishaji pamoja na bomba la kusafirisha bidhaa za mafuta linaloweza kufanya kazi kwa pande zote mbili kati ya Tanzania na Uganda.
Amesema kuwa utekelezaji wa mradi huo unalenga kuifanya Tanga kuwa kituo muhimu cha usambazaji wa bidhaa za mafuta kwa nchi za Afrika Mashariki na ukanda mpana wa Afrika.
"Utiaji saini wa leo siyo tu makubaliano, bali ni msingi mwingine wa mageuzi ya kiuchumi katika Afrika Mashariki," alisema.
Alisema mradi huo unaendeleza ushirikiano ulioanza kupitia Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), wenye thamani ya takribani dola za Marekani bilioni sita, unaolenga kusafirisha mafuta ghafi kutoka maeneo ya uzalishaji nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga.
Ndejembi alisema tofauti na EACOP ambayo inalenga kusafirisha mafuta ghafi, Kitovu cha Nishati cha Tanga kitasaidia kuongeza thamani ya rasilimali hiyo kupitia usafishaji wa mafuta, uhifadhi, usafirishaji na biashara ya bidhaa za petroli.
"Mradi huu ukikamilika una uwezo wa kuvutia uwekezaji unaozidi dola za Marekani bilioni 20, kuunda ajira, kuchochea ukuaji wa viwanda na kuimarisha usalama wa nishati katika ukanda huu," alisema.
Ndejembi aliongeza mradi huo unaendana na maono ya Rais Samia ya kuifanya Tanga kuwa kitovu cha biashara ya mafuta Afrika Mashariki kutokana na nafasi yake ya kimkakati, ikiwemo kuwa lango la Bahari ya Hindi na eneo la kupokea bomba la EACOP.
Kwa upande wake, Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini wa Uganda, Dk Ruth Nankabirwa Ssentamu, alisema makubaliano hayo yanaonyesha dhamira ya nchi hizo mbili ya kushirikiana katika kuongeza thamani ya rasilimali na kukuza uchumi wa kikanda.
"Hatupaswi kuuza malighafi pekee. Tunapaswa kujenga viwanda, kuunda ajira zenye ujuzi na kuhakikisha wananchi wetu wanapata manufaa makubwa kutokana na rasilimali hizi," alisema.
Dk Nankabirwa alisema kiwanda cha kusafisha mafuta kinachopangwa kujengwa Kabaale nchini Uganda na Kitovu cha Nishati cha Tanga havitashindana, bali vitakamilishana kwa kuongeza uwezo wa usafishaji wa mafuta na kuimarisha upatikanaji wa nishati katika Afrika Mashariki.
Aliongeza kuwa Tanzania na Uganda zinaendelea na utekelezaji wa miradi mingine ya pamoja, ikiwemo bomba la kusafirisha bidhaa za mafuta, bomba la gesi asilia kati ya nchi hizo mbili na mradi wa njia ya kusafirisha umeme wa kilovolti 400.
Utiaji saini wa makubaliano hayo ni hatua nyingine katika ushirikiano wa muda mrefu wa Tanzania na Uganda kwenye sekta ya nishati ulioimarishwa kupitia EACOP mwaka 2017.








0 Comments