Serikali kupitia Taasisi ya Uthibitishaji wa Mbegu Tanzania (TOSCI) imesisitiza umuhimu wa kulinda, kusajili na kuendeleza mbegu za asili ili kuhifadhi baionuai, kuongeza uzalishaji wa kilimo na kuhakikisha usalama wa chakula nchini.
Akizungumza leo Agosti,5 2025 jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkuu TOSCI, Nyasebwa Chimagu katika mjadala kuhusu utambuzi wa mifumo ya mbegu zinazosimamiwa na wakulima na mchango wake katika mifumo endelevu ya chakula amesema kuwa ongezeko la watu, upanuzi wa miji na mabadiliko ya matumizi ya ardhi vimechangia kupotea kwa aina mbalimbali za mimea na mbegu za asili, hali inayohitaji hatua za haraka za uhifadhi.
Alieleza kuwa mbegu ni bidhaa inayodhibitiwa kisheria kwa kuwa hutumika pia katika biashara ya ndani na nje ya nchi. Hivyo, alisema uzalishaji, usajili na usambazaji wake lazima uzingatie viwango vya ubora vilivyowekwa na sheria za Tanzania pamoja na viwango vya kimataifa.
"Mbegu bora lazima ziwe na ubora wa kijenetiki, ziwe salama dhidi ya magonjwa na ziweze kutoa mavuno yanayokidhi matarajio ya wakulima na usimamizi wa mbegu unalenga kulinda wakulima dhidi ya bidhaa zisizo na ubora.
Amesema Serikali imeanza hatua za kusajili baadhi ya mbegu za asili ili kuzitambua rasmi na kuweka utaratibu wa kuzisimamia. Alifafanua kuwa hatua hiyo itarahisisha kulinda haki za wamiliki wa mbegu hizo na kuongeza fursa za biashara.
Naye Mratibu wa Mtandao wa Baionuai Tanzania (TABIO), amesema mfumo wa sasa wa sheria za mbegu hauzitambui rasmi mbegu za wakulima, hali inayozuia kuwepo kwa utaratibu wa kuzisimamia, kuzihakiki na kuzilinda kisheria.
Amesema Sheria ya Mbegu ya mwaka 2003 pamoja na marekebisho yake na Kanuni za mwaka 2017 zimejikita zaidi katika mbegu zilizothibitishwa, huku mbegu za wakulima zikikosa utambuzi wa moja kwa moja na hivyo kutoruhusiwa kuuzwa kwa kuwa hazijathibitishwa na mamlaka husika.
"Tofauti na mbegu rasmi ambazo zina mfumo maalumu wa utafiti, uhakiki na udhibiti wa ubora, mbegu za wakulima zinazochangia zaidi ya asilimia 60 ya mbegu zinazotumiwa nchini bado hazina utaratibu rasmi wa kuhakikisha ubora wake,"amesema.
Aidha, ameeleza kuwa kuna haja ya kuimarisha ulinzi wa haki za wakulima ambao wamekuwa wakihifadhi, kubadilishana na kuendeleza mbegu za asili kwa vizazi vingi, pamoja na kuweka utaratibu wa kuhakikisha wanapata manufaa pale mbegu hizo zinapotumika katika tafiti au kuboreshwa.
Ametoa wito kwa Serikali na wadau wa sekta ya kilimo kukamilisha mfumo wa uhakiki na usimamizi wa ubora wa mbegu za wakulima ili uweze kuwasilishwa kwa mamlaka husika kwa ajili ya kufanyiwa kazi na kuingizwa katika mfumo rasmi wa usimamizi wa mbegu nchini.
Katika mjadala huo, wadau wa kilimo walieleza kuwa mfumo wa sasa wa sheria bado haujatambua kikamilifu mbegu zinazosimamiwa na wakulima, jambo linalozuia maendeleo ya sekta hiyo na kupunguza fursa za wakulima kunufaika na rasilimali walizozihifadhi kwa miaka mingi.
Walidai kuwa kuna haja ya kuweka mfumo rasmi wa kuhakiki ubora wa mbegu za wakulima, sambamba na kulinda haki zao za kuzalisha, kuhifadhi, kubadilishana na kuuza mbegu kwa mujibu wa sheria
Wataalamu pia walieleza kuwa mbegu za asili zina uwezo mkubwa wa kustahimili mazingira magumu ikiwemo ukame, hivyo zina mchango muhimu katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kuhakikisha upatikanaji wa chakula.
Aidha, ilielezwa kuwa tafiti shirikishi zinazowashirikisha wakulima zina mchango mkubwa katika kutambua, kuhifadhi na kuboresha mbegu za asili, huku zikiwapa wakulima nafasi ya kutambua haki zao na kushiriki katika maamuzi kuhusu rasilimali hizo.
Wawakilishi wa mashirika ya kilimo hai Afrika walisema ushirikiano wa kikanda unaweza kuongeza masoko ya mbegu za asili, kurahisisha ubadilishanaji wa mbegu kati ya nchi na kusaidia kuhifadhi aina mbalimbali za mazao yanayokaribia kutoweka.
Wadau hao walihitimisha kwa kuitaka Serikali kuimarisha mfumo wa sheria na taasisi zinazoshughulikia mbegu ili kuwe na mfumo unaoaminika wa kudhibiti ubora wa mbegu zinazosimamiwa na wakulima na kuhakikisha zinachangia maendeleo ya kilimo endelevu nchini.
Mjadala huo ulihitimishwa kwa wito kwa Serikali, taasisi za utafiti, mashirika ya kiraia na wakulima kuendelea kushirikiana katika kulinda mbegu za asili, ambazo zimeelezwa kuwa msingi wa usalama wa chakula, uhifadhi wa bioanuwai na maendeleo ya uchumi wa kilimo nchini.





0 Comments