Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Deus Sangu,akiwahutubia washiriki wa mafunzo ya usalama na afya mahali pa kazi yaliyotolewa na OSHA katika Mgodi wa Namungo uliopo Wilaya ya Ruangwa Mkoani Lindi.
**************
Na Mwandishi Wetu
Wachimbaji wadogo wa Mgodi wa Namungo wameiomba Serikali kupitia Wakala waUsalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) kuwapatia mafunzo ya usalama na afya mahali pa kazi mara kwa mara ili waweze kutekeleza shughuli za uchimbaji na uchakataji madini kwa kuzingatia kanuni bora za usalama na afya mahali pa kazi.
Wamewasilisha maombi hayo baada ya kushiriki mafunzo ya usalama na afya yaliyoandaliwa na OSHA kwa wachimbaji wadogo zaidi ya 400 wanaofanya shughuli zao katika Mgodi wa Namungo.
Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wakiwemo Ramadhan Abdallah na Salum Mfaume wamesema wamejifunza mambo mengi muhimu kupitia mafunzo hayo yaliyotolewa kwao Agosti 4, 2026 ambapo wamesisitiza kwamba mafunzo hayo yatabadilisha utamaduni wa kutozingatia tahadhari katika shughuli zao za kila siku.
“Kwasiku ya leo tunashukuru ujio wa OSHA ambao wametupa elimu ambayo itatusaidiasana katika shughuli zetu za kila siku lakini pia elimu ambayo tunatakiwa kuendelea kuizingatia ili iweze kutuletea manufaa. Tunawashukuru sana na pia tunawaomba muendelee kutupatia mafunzo haya mara kwa mara,” amesema Ramadhani Abdallah.
“Binafsi nawashukuru OSHA kwa kuja kututembelea leo, kifupi tumejifunza mambo mengi sana kupitia wao hivyo tunaomba isiwe mwisho leo na tunaomba utaratibu huuuwe endelevu katika vipindi tofauti tofauti,” ameeleza Salum Mfaume.
Akisoma risala ya wachimbaji hao mbele ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Deus Sangu, Katibu wa Chama cha Wachimbaji Namungo, Bw. Emmanuel Johanes amesema wamepata mafanikio makubwa katika shughuli za uchimbaji madini kutokana na ushirikiano uliopo baina yao na Taasisi za serikaliikiwemo OSHA.
“Kampuni ya Elianje Genisis inayomiliki leseni ya eneo hili tunalofanya shughuli zetu za uchimbaji imefanya maboresho makubwa sana katika miundombinu ya uchimbaji kwakuweka kiupaumbele katika usalama, afya na ulinzi wa wafanyakazi. Maboresho hayo yamefanyika kwa ushirikiano na Taasisi mbalimbali za serikali ikiwemo OSHA. Hatua hiiimetokana na imani yetu kwamba maisha ya wafanyakazi yana thamani kubwa kuliko uzalishaji wowote unaoweza kufanyika,” ameeleza Bw. Emmanuel Johanes.
Akiwahutubia washiriki wa mafunzo hayo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Deus Sangu, amesema mafunzo ya usalama na afya ni muhimu ili kuwawezesha wachimbaji kuchukua tahadhari dhidi vihatarishi vingi vilivyopo katika shughuli za uchimbaji madini.
Aidha, amebainisha kwamba mafunzo hayo yametolewa kwa muda mfupi hivyohayawezi kukidhi mahitaji ya elimu ya usalama na afya kwa wachimbaji hao ambapo ameahidi kumwelekeza Mtendaji Mkuu wa OSHA kuandaa mafunzo zaidi kwa ajili yakundi hilo lenye wachimbaji wadogo zaidi ya 4,000.
Mgodi wa Namungo unamilikiwa na Kampuni ya Elianje Genesis ambayo imetoa nafasikwa wachimbaji wadogo kufanya shughuli zao ndani ya mgodi huo na kuuza madini kwa kampuni hiyo. Madini yanayopatikana katika mgodi huo ni pamoja na dhahabu, green garnet pamoja na grahite.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Deus Sangu,akiwahutubia washiriki wa mafunzo ya usalama na afya mahali pa kazi yaliyotolewa na OSHA katika Mgodi wa Namungo uliopo Wilaya ya Ruangwa Mkoani Lindi.
Meneja wa OSHA Kanda ya Kusini, Mhandisi Uswege Faston (wakwanza kushoto), akifuatilia hotuba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Deus Sangu, alipohitimisha mafunzo ya siku moja ya usalama na afya kazini yaliyotolewa na OSHA kwa wachimbaji wadogo wa Mgodi wa Namungo uliopo Ruangwa Mkoani Lindi.
Wachimbaji wadogo wa Mgodi wa Namungo wakisikiliza mada mbalimbali katika mafunzo maalum ya usalama na afya mahali pa kazi yaliyotolewa na OSHA katika Mgodi huo uliopo Wilaya ya Ruangwa Mkoani Lindi.
Mkufunzi wa OSHA, Bi. Moteswa Meda, akiwasilisha mada kuhusu Misingi ya Huduma ya Kwanza Mahali pa Kazi (kwa nadharia na vitendo) katika mafunzo ya usalama na afya yaliyoandaliwa na OSHA kwa ajili ya wachimbaji wadogo wa Mgodi wa Namungo uliopo Ruangwa Mkoani Lindi.
Afisa Mafunzo Mwandamizi wa OSHA, Bw. Simon Lwaho, akiwasilisha mada kuhusu vihatarishi vya usalama na afya mahali pa kazi katika mafunzo yaliyoandaliwa na OSHA kwa ajili ya wachimbaji wadogo wa Mgodi wa Namungo uliopo Ruangwa Mkoani Lindi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano), Deus Sangu, akikabidhi baadhi ya vifaa kinga vilivyotolewa na OSHA sambamba na mafunzo ya usalama na afya mahali pa kazi kwa wachimbaji wadogo wa Mgodi wa Namungo uliopo Wilaya ya Ruangwa Mkoani Lindi.
Baadhi ya wachimbaji wadogo wakipata huduma ya uchunguzi wa afya zao ikiwa ni sehemu ya program ya mafunzo na uhamasishaji masuala ya usalama na afya kazini iliyoandaliwa kwa ajili yao na OSHA.













0 Comments