Ticker

6/recent/ticker-posts

WADAU WATAKA TUME HURU YA MARIDHIANO, WAPENDEKEZA MCHAKATO WA KATIBA MPYA UFUFULIWE

 

Na Mwandishi Wetu

Wadau kutoka sekta mbalimbali nchini wamependekeza kuundwa kwa tume huru ya maridhiano itakayoshirikisha wataalamu wa kimataifa kwa lengo la kutibu majeraha ya kijamii, kuimarisha ustahimilivu na kurejesha amani nchini.

Mapendekezo hayo ni sehemu ya maazimio yaliyotolewa na washiriki wa maadhimisho ya Siku ya Wanawake wa Kiafrika yaliyofanyika mwishoni mwa wiki na kuandaliwa na Shirika la Women in Law and Development in Africa (WiLDAF).

Aidha, wadau hao walisisitiza kuwa baada ya maridhiano kufikiwa, itungwe sheria mpya ya kuanzisha upya mchakato wa kupata Katiba ya wananchi, huku wakipendekeza mchakato huo uendelee kuanzia ulipokuwa umeishia.

Katika maazimio hayo, washiriki walipendekeza pia kufanyika kwa kura ya maoni ili wananchi wachague kati ya Rasimu ya Katiba iliyotokana na Tume ya Jaji Joseph Warioba na Katiba Iliyopendekezwa na Bunge Maalumu la Katiba, kwa kuzingatia pia mustakabali wa Muungano.

Vilevile, wadau walishauri kuundwa kwa jopo la wataalamu huru wasiofungamana na vyama vya siasa kutoka nchi mbalimbali ili kusaidia kusimamia mchakato wa maridhiano na ule wa uandaaji wa Katiba.

Maadhimisho hayo yaliwakutanisha washiriki kutoka vyama vyote 19 vya siasa vilivyosajiliwa nchini, watetezi wa haki za wanawake, wanachama wa Mtandao wa Kupinga Ukatili Nchini, MKUKI, majaji, wanasheria, wadau wa maendeleo, mashirika ya kitaifa na kimataifa, wawakilishi wa Umoja wa Mataifa pamoja na wahadhiri kutoka vyuo vikuu mbalimbali nchini.





























































































Post a Comment

0 Comments