
Na WMA - DODOMA.
Wajasiriamali wa kikundi cha Hapa Kazi kutoka Shehia ya Mtemani Wingwi, Wilaya ya Micheweni, Mkoa wa Kaskazini Pemba wametembelea banda la Wakala wa Vipimo (WMA) katika Maonesho ya 33 ya Wakulima Nane Nane yanayofanyika Viwanja vya Dkt. John Samwel Malecela, Nzuguni, jijini Dodoma.
Katika ziara hiyo iliyofanyika leo Agosti 6, 2026, wajasiriamali hao wameshukuru kupata elimu kuhusu matumizi sahihi ya vipimo, ufungashaji bora wa bidhaa na mbinu za kuongeza ushindani wa bidhaa zao sokoni.

Mwakilishi wa kikundi hicho, Asha Mwiaka Haji, amesema maonesho hayo yameendelea kuwafungua macho na kuwaongezea uelewa mkubwa kuhusu vigezo vinavyopaswa kuzingatiwa katika biashara ili bidhaa zao ziweze kupenya kwenye masoko.
“Tumefurahi sana kufika banda la WMA maana sisi pia tuna Wakala kama hii Zanzibar. Tumejifunza jinsi ya kutumia mizani, kuweka lebo sahihi na umuhimu wa vipimo katika biashara yetu, elimu ambayo pia tumekuwa tukiipata kupitia Wakala yetu ya Vipimo Zanzibar,” alisema.
Asha ameeleza kuwa kikundi chao kinajishughulisha na usindikaji na uuzaji wa bidhaa mbalimbali zikiwemo mwani, mafuta ya mgando, sabuni za mwani pamoja na dawa za asili.
Aidha, amesema ushiriki wao katika maonesho hayo umewaongezea ujuzi na uelewa zaidi kuhusu matumizi sahihi ya vipimo, mfumo wa alama za mistari (barcodes) na mbinu bora za kufungasha bidhaa.
“Tunawashukuru WMA kwa elimu hii. Tukirudi kwetu, tutaendelea kuwaelimisha pia wajasiriamali wengine ili tuweze kuzalisha bidhaa zenye ubora na zinazokidhi viwango vya soko,” alisema Asha.
Aidha, Asha amewahimiza wajasiriamali wenzake kushirikiana kwa karibu na maafisa wa Serikali katika ngazi ya shehia na wilaya ili kubuni mikakati itakayoongeza thamani ya bidhaa zao na kuchochea ukuaji wa uchumi.
Wakala wa Vipimo (WMA) inafanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na Wakala wa Vipimo Zanzibar (ZAWEMA)

0 Comments