Na Mwandishi Wetu.Dar es Salaam, 5 Septemba 2026 – Benki ya CRDB kwa kushirikiana na TRA SACCOS imezindua rasmi TRA SACCOS PESACARD, kadi mpya inayotumia mfumo wa Visa inayolenga kuwapa wanachama wa TRA SACCOS urahisi, uhuru na wigo mpana zaidi wa kupata na kutumia fedha zao, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 20 ya TRA SACCOS.
Uzinduzi huo ni hatua muhimu katika ushirikiano wa muda mrefu kati ya Benki ya CRDB na TRA SACCOS, na unaashiria awamu mpya ya mageuzi ya kidijitali katika utoaji wa huduma za kifedha kwa wanachama wa SACCOS hiyo.
Kupitia TRA SACCOS PESACARD, wanachama wataunganishwa na mfumo mpana wa malipo wa Visa na hivyo kuwa na uwezo wa kutoa fedha kupitia ATM pamoja na kufanya malipo katika vituo vya POS vinavyokubali Visa ndani na nje ya Tanzania.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo aliipongeza TRA SACCOS kwa kufikisha miaka 20 tangu kuanzishwa kwake, huku akiipongeza Benki ya CRDB kwa kuendelea kutumia uwezo wake wa kiteknolojia na kifedha kusaidia taasisi mbalimbali kupanua huduma za kisasa za kifedha.
“Miaka 20 ni hatua kubwa inayodhihirisha uimara, uaminifu na mchango wa TRA SACCOS katika kuboresha ustawi wa kifedha wa wanachama wake. Nawapongeza viongozi na wanachama kwa kuendelea kubadilika kulingana na mahitaji ya wakati, na Benki ya CRDB kwa kutumia uwezo wake wa kifedha na kiteknolojia kujenga ushirikiano unaorahisisha upatikanaji wa huduma. Uzinduzi wa TRA SACCOS PESACARD unaonesha mafanikio tunayoweza kuyapata pale taasisi za fedha na vyama vya ushirika vinapounganisha nguvu katika kukuza ubunifu na ujumuishi wa kifedha.”
Pamoja na uzinduzi wa kadi hiyo, ushirikiano huo umewezesha kuunganishwa moja kwa moja kwa mifumo ya TRA SACCOS na mifumo ya Benki ya CRDB. Maboresho hayo yanamaanisha kuwa mwanachama anaweza kutumia akaunti yake iliyopo ndani ya mfumo wa TRA SACCOS kupata huduma zinazohusiana na PESACARD bila kulazimika kuwa na akaunti katika benki nyingine ya biashara.
Muunganiko huo pia unatarajiwa kuongeza ufanisi katika utoaji wa mikopo kwa wanachama. Fedha za mikopo zitaweza kutolewa moja kwa moja kupitia mfumo wa TRA SACCOS, hatua inayopunguza michakato ya kuhamisha fedha kutoka mfumo mmoja kwenda mwingine na hivyo kupunguza muda wa mwanachama kusubiri fedha baada ya mkopo wake kuidhinishwa.
Katibu wa Benki ya CRDB, Pascal Mihayo, alisema hatua hiyo inaakisi dhamira ya Benki ya kutumia teknolojia na ushirikiano wa kimkakati kutengeneza suluhisho zinazojibu mahitaji halisi ya wateja.
“Kwetu Benki ya CRDB, huu ni zaidi ya uzinduzi wa kadi. Ni uthibitisho wa namna ushirikiano wa muda mrefu unavyoweza kukua na kuzaa suluhisho zinazogusa maisha ya watu moja kwa moja. Kupitia TRA SACCOS PESACARD na muunganiko wa mifumo yetu, tunawapa wanachama uhuru zaidi wa kupata na kutumia fedha zao, huku tukiiwezesha TRA SACCOS kuongeza kasi na ufanisi wa utoaji wa huduma. Haya ndiyo mageuzi ya kidigitali tunayoyasimamia, teknolojia inayorahisisha huduma, inayozisogeza karibu na wananchi na inayoongeza thamani halisi kwa mtumiaji.”
Miongoni mwa maboresho mengine muhimu ni kuunganishwa kwa huduma za TRA SACCOS na mtandao wa Mawakala wa CRDB. Hatua hiyo itawawezesha wanachama kuweka na kutoa fedha kupitia zaidi ya Mawakala 40,000 wa CRDB waliopo maeneo mbalimbali nchini, hivyo kupanua kwa kiasi kikubwa maeneo ambayo mwanachama anaweza kupata huduma.
Maboresho hayo yana umuhimu mkubwa hususan kwa wanachama waliopo nje ya maeneo yenye matawi ya benki, kwa kuwa yanapunguza utegemezi wa maeneo ya kawaida ya huduma za kifedha na kutumia mtandao mpana wa Benki ya CRDB kupeleka huduma karibu zaidi na mwanachama.
Kwa upande wake, Kamishnawa TRA, Yusuph Mwenda aliishukuru Benki ya CRDB kwa ushirikiano wake, akieleza kuwa PESACARD na muunganiko wa mifumo ni sehemu muhimu ya safari ya TRA SACCOS ya kuboresha na kufanya huduma zake kuwa za kisasa zaidi.
“Tunapoadhimisha miaka 20 ya TRA SACCOS, hatuangalii tu tulikotoka na mafanikio tuliyoyapata; tunaangalia pia tunakotaka kwenda na aina ya taasisi tunayotaka kuijenga kwa ajili ya wanachama wetu. TRA SACCOS PESACARD ni sehemu ya safari hiyo ya baadaye. Inawapa wanachama wetu urahisi, wigo mpana zaidi wa huduma na uwezo mkubwa wa kusimamia miamala yao. Tunaishukuru Benki ya CRDB kwa kuamini maono yetu na kushirikiana nasi kuleta teknolojia inayoongeza uwezo wetu wa kuwahudumia wanachama vizuri zaidi.”
Uzinduzi wa TRA SACCOS PESACARD pia unaonesha umuhimu wa ushirikiano kati ya benki za biashara na taasisi za kifedha zinazomilikiwa na wanachama katika kuongeza ujumuishi wa kifedha. Kwa kuunganisha ukaribu wa TRA SACCOS na wanachama wake pamoja na teknolojia, miundombinu na uwezo wa malipo wa Benki ya CRDB, ushirikiano huo unalenga kuunda mazingira rahisi zaidi ya kupata huduma za kisasa za kifedha.
Kwa Benki ya CRDB, hatua hiyo ni sehemu ya dhamira yake ya kuendelea kuwekeza katika teknolojia na kubuni suluhisho zinazoboresha uzoefu wa wateja na kupanua upatikanaji wa huduma za kifedha. Benki hiyo imeahidi kuendelea kushirikiana na TRA SACCOS pamoja na taasisi nyingine katika sekta binafsi na umma kuleta mageuzi ya kidigitali na katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
0 Comments