
Wananchi wanaoishi maeneo mbalimbali kuzunguka Hifadhi ya Taifa Tarangire imeadhimisha Siku ya Utalii Duniani kwa matembezi ya hisani ya baiskeli ya kilomita 10, ikiwan ni sehemu ya kuhamasisha shughuli za utalii.
Matembezi hayo yalifanyika Septemba 27, 2026, huku washiriki pia wakipata fursa ya kujionea vivutio mbalimbali vinavyopatikana ndani ya hifadhi hiyo iliyopo wilaya ya Babati mkoani Manyara, kaskazini mwa Tanzania.
Matembezi hayo yaliongozwa na Kamishna Mwandamizi Msaidizi wa Uhifadhi na Mkuu wa Kanda ya Kaskazini, Dkt. Noelia Myonga.
Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Tarangire, Dkt. Tutindaga George, alisema utalii ndani ya hifadhi hiyo ni fursa muhimu ya kuongeza uchumi wa mtu mmoja mmoja, jamii na taifa kwa ujumla.
Dkt. Tutindaga alisema uwepo wa hifadhi hiyo umesaidia kwa kiasi kikubwa kuinua sekta ya utalii wilayani Babati na hivyo kuwataka wananchi, hasa vijana, kuchangamkia fursa hiyo ili kuboresha maisha yao.
Naye Diwani wa Kata ya Mamire, Augustine Sosie, alisema eneo lote linalozunguka lango la Mamire linafaa kwa uwekezaji wa shughuli mbalimbali za kitalii.
Mratibu wa matembezi hayo, Elizabeth Yusufu, aliunga mkono kauli ya Dkt. Tutindaga ya kuwataka vijana kuchangamkiq fursa ya kunufaika na shughuli za utalii kama vile kufanya biashara.
Dkt. Tutindaga (katikati aliyevaa kofia nyeupe) na wafanyakazi wa Hifadhi ya Tarangire wakifurahia picha ya pamoja na washiriki wengine wa matembezi hayo.
Akizungumza kwenye maadhimisho hayo ya Siku ya Utalii Duniani, mwakilishi wa Kampuni ya Utalli ya Swala Camp, Walter Pallangyo, alitilia mkazo umuhimu wa Watanzania kutunza mazingira na kuwapenda wanyamapori kama zawadi mahsusi kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa taifa hili kubwa la Afrika Mashariki.
Kaulimbiu ya maadhimisho ya Siku ya Utalii Duniani mwaka huu wa 2026 inasema: "Ajenda ya Kijiditali na Akili Bandia Kubuni Upya Sekta ya Utalii".
Msisitizo mkubwa umewekwa kwenye kuwahamasisha Watanzania kutembelea Hifadhi ya Taifa Tarangire badala ya kubaki kuwa watazamaji kwa kuwaachia wageni fursa hiyo.


























0 Comments