-Atoa siku saba Kupatikana kwa Suluhisho la Mgogoro wa Udhibiti wa Taka
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius John Ndejembi, amefanya ziara katika Dampo la Pugu Kinyamwezi jijini Dar es Salaam, ambapo amekagua hali ya udhibiti na usimamizi wa taka.
Katika ziara hiyo, ameambatana na viongozi wa Halmashauri za Jiji la Dar es Salaam, viongozi wa Ofisi yake, Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dkt. Immaculate Sware Semesi, pamoja na baadhi ya watumishi wa taasisi hiyo.
Mhe. Ndejembi amewaagiza viongozi wa Halmashauri za Jiji la Dar es Salaam, Wizara na taasisi husika kukutana na kujadili kwa kina njia bora na endelevu za kudhibiti taka katika dampo hilo.
Amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa karibu miongoni mwa wadau hao ili kupata ufumbuzi wa kudumu wa changamoto zinazolikabili eneo hilo.
Katika kutekeleza maagizo hayo, ameelekeza viongozi hao kufikia makubaliano kuhusu njia bora za udhibiti wa taka na kuwasilisha kwake ripoti yenye mapendekezo ndani ya siku saba.
Aidha, ameagiza kupuliziwa dawa maalum dhidi ya vimelea vya magonjwa katika maeneo yanayolizunguka dampo, hususan makazi ya wananchi walio jirani, ili kupunguza hatari ya kuenea kwa magonjwa yanayoweza kusababishwa na taka.
Sambamba na hilo, Makamu wa Rais amewataka viongozi na taasisi zinazohusika kushirikiana katika ukusanyaji na uwasilishaji wa takwimu sahihi za taka, ili taarifa zinazotolewa ziwe na uhalisia na kuendana.








0 Comments