NA: DK. REUBENI LUMBAGALA
Serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetoa tafsiri ya mfanyabiashara mdogo kwa muktadha wa ulipajikodi. Mfanyabiashara mdogo ni mtu anayeuza bidhaa au huduma ambaye mauzo yake kwa mwaka mzima ni kati ya shilingi sifuri hadi milioni 200.
Kimsingi, mfanyabiashara mdogo, wa kati na mkubwa, wote kwa pamoja wanao wajibu wa kulipa kodi kwa ajili ya kuchangia maendeleo ya nchi.
Lakini yapo mabadiliko ya sheria za kodi yaliyofanyika kwa mwaka wa fedha 2026/2027, ambayo yamempa ahueni mfanyabiashara mdogo anayeanza biashara kupata msamaha wa kodi kwa kipindi cha mwaka mmoja (miezi 12). Lengo lake ni kumwezesha mfanyabiashara huyo kujijenga kibiashara kwanza ili baadaye aweze kumudu kulipa kodi bila usumbufu.
Ni kwamba, mfanyabiashara mdogo anayeanza biashara, mwenye Namba mpya ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN), ambaye mauzo yake ni kati ya shilingi sifuri hadi milioni 200, amepewa msamaha wa kodi kwa muda wa mwaka mzima.
Mabadiliko haya yamekuja kutokana na maoni ya wadau mbalimbali ambao wamekuwa wakishauri umuhimu wa kutoa msamaha wa kodi kwa wafanyabiashara wadogo wapya ili wajijenge kibiashara kabla ya kuanza kulipa kodi.
Awali, wafanyabiashara wadogo walikuwa wakikabiliwa na ugumu wa kulipa kodi kwa wakati kutokana kudaiwa kodi na TRA kipindi ambacho biashara zao hazijastawi na hivyo kushindwa kulipa kodi.
Hii ilisababisha baadhi yao kufunga biashara huku wakiwa na deni la kodi. Pia, iliwapoteza kabisa wafanyabiashara katika ramani ya kufanya biashara. Waliyumba kiuchumi na kupoteza mwelekeo wa kibiashara kabisa.
Kutokana na kilio hicho, serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, ikaridhia mabadiliko ya sheria za kodi ili kutoa unafuu. Hapa matumaini mapya ya kuinuka kibiashara yakafufuka upya.
Ukweli ni kwamba, serikali imechukua jukumu la mzazi, yaani kuwalea na kuwaatamia wafanyabiashara wadogo kwa kuwawekea mazingira mazuri na wezeshi ili wasiwe na msongo wa mawazo (stress) wa kulipa kodi katika kipindi cha mwaka mzima na badala yake waongeze juhudi za kufanya biashara tu na kujiingizia kipato.
Ni vyema kwa wananchi wote wenye dhamira ya kuanza biashara, kuondoa hofu na badala yake waitumie vyema fursa hii ya msamaha wa kodi iliyotolewa na serikali ili waweze kuanzisha bishara hatimaye waweze kujiingizia kipato na kuchagia maendeleo ya nchi.
Msamaha wa kodi wa mwaka mzima ni nyenzo muhimu ya kuongeza idadi ya wafanyabiashara nchini ambao ni muhimu katika kukuza uchumi na maendeleo.
Aidha, msamaha huu utakapomalizika, wafanyabiashara wanufaika wataingia rasmi katika mfumo wa ulipajikodi, ambapo watakuwa wadau muhimu katika kuchechemua uchumi na maendeleo kwa ujumla kwani kodi zao zitatumika kuboresha sekta mbalimbali za maendeleo kama vile elimu, afya, kilimo, umeme, biashara, viwanda, maji, miundombinu, masoko, uvuvi, madini na utalii.

0 Comments