TANZANIA inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Pili wa Afrika na Nchi za Ghuba (GCC Plus), unaojulikana kama Doha Dialogue, utakaofanyika Oktoba 5 na 6, 2026, jijini Dar es Salaam, ukilenga kuimarisha ushirikiano katika uhamaji wa wafanyakazi, ajira na mahitaji ya soko la ajira.
Mkutano huo utawakutanisha nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU), nchi sita za Baraza la Ushirikiano la Nchi za Ghuba (GCC)—Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Qatar, Kuwait, Oman na Bahrain pamoja na Jordan na Lebanon.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 28, 2026 jijini Dar es Salaam, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu, amesema mkutano huo utakuwa jukwaa la kujadili mikakati ya pamoja ya kuhakikisha uhamaji wa wafanyakazi unakuwa salama, wenye tija na unaozingatia haki zao.
Amesema mkutano huo pia utajadili namna ya kukuza fursa za ajira, hususan kwa vijana, pamoja na kuimarisha ulinganifu kati ya ujuzi wa wafanyakazi na mahitaji ya soko la ajira katika nchi za Afrika na Mataifa ya Kiarabu.
Mkutano wa kwanza ulifanyika Doha, Qatar, Mei 21 na 22, 2024, ukihudhuriwa na nchi 43, zikiwemo 25 za Afrika, nchi za GCC, Jordan na Lebanon.
“Tanzania ilishiriki katika mkutano huo wa kwanza ambao ulihusisha majadiliano yaliyolenga kuimarisha ushirikiano kati ya nchi za Afrika na nchi za Kiarabu katika masuala ya uhamaji wa wafanyakazi,” amesema Sangu.
Amesema mkutano huo ulihitimishwa kwa kupitishwa kwa Azimio la Doha (Doha Declaration), lililoweka msingi wa kuendeleza majadiliano na ushirikiano kati ya pande hizo.
Aidha amesema, Tanzania imepata nafasi ya kuwa nchi ya pili kuwa mwenyeji wa mkutano huo unaofanyika kila baada ya miaka miwili, na utakuwa wa kwanza kufanyika katika bara la Afrika.
Amesema moja ya maeneo yatakayojadiliwa ni makubaliano ya uhamaji wa wafanyakazi, ujuzi, mahitaji ya soko la ajira na uanzishwaji wa mifumo ya kuhakikisha uhamaji unakuwa salama na wenye tija.
Akizungumzia fursa za ajira nje ya nchi, Waziri Sangu amesema Serikali imeweka mifumo ya kuhakikisha Watanzania wanaokwenda kufanya kazi nje ya nchi wanapitia taratibu rasmi na kupata mikataba inayolinda haki zao.
Amesema mikataba hiyo inalenga kuweka wazi viwango vya mishahara, aina ya kazi wanayopangiwa pamoja na mazingira ya ajira, huku Serikali ikichukua hatua za kuwalinda dhidi ya unyanyasaji na vitendo vya kunyang’anywa hati zao za kusafiria.
“Katika Wizara kwa sasa hakuna mfanyakazi anayefanya kazi nchini bila kupitia kwenye mfumo wa Wizara. Wote tumewapa mawasiliano, wana mawasiliano ya balozi na wana mawasiliano ya Wizara. Lengo ni kuhakikisha kama changamoto yoyote inatokea wawe tayari kutujulisha mara moja na hatua stahiki zichukuliwe,” amesema.
0 Comments