Na OWM–TAMISEMI, Arusha
Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuimarisha huduma za afya ngazi ya jamii kupitia mifumo ya kidijitali ya malipo na taarifa, ambayo imeboresha utambuzi, usimamizi, ufuatiliaji na ulipaji wa wahudumu wa afya ngazi ya jamii.
Mkurugenzi wa Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Huduma za Lishe, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OWM - TAMISEMI), Dkt. Rashid Mfaume, ameyasema hayo Septemba 10, 2026, wakati akichangia mada kuhusu safari ya Tanzania ya kuwalipa wahudumu hao kidijitali katika Mkutano wa Kimataifa wa Afya ya Msingi (IPHC), unaoendelea katika Ukumbi wa AICC Jijini Arusha.
Dkt. Mfaume amesema kabla ya kuanzishwa rasmi kwa Programu Jumuishi na Iliyoratibiwa ya Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii, Januari 2024, usimamizi wa wahudumu zaidi ya 55,000 nchini ulikuwa umegawanyika.
Washirika wa maendeleo waliwapa majina, majukumu, mifumo ya taarifa na taratibu tofauti za malipo, hali iliyofanya uratibu na uthibitishaji wa taarifa kuwa mgumu.
Ameeleza kuwa kuunganishwa kwa mifumo ya malipo ya kidijitali na mifumo shirikishi ya taarifa za rasilimali watu kumeiwezesha Serikali kuwatambua wahudumu, kuthibitisha sifa zao za kupata malipo na kufuatilia utendaji wao kwa ufanisi.
“Kupitia dashibodi ya kidijitali, tunaweza kubaini anayestahili kulipwa, kufuatilia maendeleo ya kazi na kutoa msaada kuanzia ngazi ya kituo cha afya hadi wizara,” amesema.
Dkt. Mfaume amesema mfumo huo umefanikiwa kufikisha malipo kwa asilimia 82 ya wahudumu na kuimarisha usimamizi saidizi katika ngazi zote. “Changamoto chache zilizopo hazipaswi kuturudisha nyuma; tunapaswa kuzitatua kwa pamoja kama Tanzania, Afrika na jumuiya ya kimataifa,” amesisitiza.
Naye Mhudumu wa Afya Ngazi ya Jamii, Bi Farida Mvungi, akitoa ushuhuda wa ufanisi wa program hiyo ya malipo, ameishukuru Serikali kwa kuwapatia posho ya Shilingi 100,000 na kupitia simu za mkononi anaona ujumbe moja kwa moja, tofauti na awali walipolazimika kufuatilia malipo kwa wahusika.



0 Comments