Ticker

6/recent/ticker-posts

Ad Code

Responsive Advertisement

WADAU WA USAFIRISHAJI WAKUTANA KUIMARISHA BIASHARA YA KIKANDA



Kigoma, Septemba 16, 2026

Wadau mbalimbali wa sekta ya Uchukuzi na Usafirishaji wamekutana mjini Kigoma katika kikao cha siku moja kilichoandaliwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), kwa lengo la kujadili fursa na changamoto zinazohusiana na usafirishaji wa mizigo na namna ya kuimarisha biashara katika ukanda wa Magharibi na Maziwa Makuu.

Kikao hicho kimehudhuriwa na wadau mbalimbali kutoka katika sekta ya Uchukuzi na Usafirishaji, ambapo Mgeni Rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Dkt. Rashid Chuachua, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano miongoni mwa wadau katika kuimarisha ufanisi wa usafirishaji na kukuza biashara ya kikanda.

Kwa upande wa TPA, Naibu Mkurugenzi Mkuu, Mha. Dkt. Baraka Mdima, ameshiriki kikao hicho kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TPA, akiwakilisha uongozi wa Mamlaka katika majadiliano yaliyolenga kubaini maeneo ya kimkakati ya kuboresha huduma na kuongeza ufanisi wa usafirishaji kupitia Bandari ya Kigoma.

Majadiliano katika kikao hicho yamejikita katika kubaini changamoto zinazokwamisha mtiririko wa mizigo, zikiwemo vikwazo visivyo vya kiforodha, ucheleweshaji na gharama za usafirishaji, pamoja na kutafuta suluhu za pamoja zitakazoboresha mazingira ya biashara na kuongeza ushindani wa njia za usafirishaji.

Aidha, wadau wamejadili umuhimu wa kuimarisha matumizi ya Bandari ya Kigoma kama lango muhimu la biashara katika ukanda wa Maziwa Makuu, hususan kupitia Ushoroba wa Kati (Central Corridor) unaoiunganisha Tanzania na nchi jirani.

Kikao hicho pia kimekuwa fursa ya kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, sekta binafsi na wadau wengine wa mnyororo wa usafirishaji katika kuboresha huduma, kupunguza muda na gharama za usafirishaji, na kuweka mazingira rafiki zaidi kwa biashara ya ndani na ya kikanda.

Kwa ujumla, kikao hicho kimeendelea kuonesha umuhimu wa majadiliano ya pamoja katika kutatua changamoto za usafirishaji na kutumia fursa zilizopo katika ukanda wa Magharibi, huku Bandari ya Kigoma ikiendelea kuwa sehemu muhimu ya kuunganisha biashara ya Tanzania na masoko ya nchi za Maziwa Makuu.

















Post a Comment

0 Comments