Ticker

6/recent/ticker-posts

Ad Code

Responsive Advertisement

DIT YAPOKEA WANAFUNZI WAPYA 2026/2027, 7,000 WANATARAJIWA KUJIUNGA NA TAASISI HIYO

  Na Mwandishi Wetu.

Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) imeanza kupokea na kutoa mafunzo ya utambulisho    ( Orientation )  kwa wanafunzi wapya wa mwaka wa masomo 2026/2027 katika kampasi zake za Dar es Salaam, Mwanza na Songwe.

Akizungumza kuhusu zoezi hilo, Mkuu wa Kitengo cha Udahili wa DIT, Dkt. Triphonia Ngailo, amesema kuwa kupitia mafunzo ya utambulisho, wanafunzi wanapewa taarifa na maelekezo muhimu yatakayowawezesha kuifahamu taasisi hiyo, taratibu zake pamoja na wajibu wao katika kipindi chote cha masomo.

Amesema mafunzo hayo yanahusisha kanuni na taratibu mbalimbali za taasisi, ikiwemo masuala ya kitaaluma, udahili, mitihani, afya na huduma zinazolenga kuwasaidia wanafunzi kukabiliana na changamoto za kisaikolojia wanapokuwa chuoni.



Aidha, Dkt. Ngailo amesisitiza umuhimu wa wanafunzi kufuata utaratibu rasmi wa malipo, akieleza kuwa malipo yanayohusiana na taasisi hiyo yanapaswa kufanyika kwa kutumia *Control Number* inayotolewa na DIT ili kuhakikisha taratibu za malipo zinafuatwa kwa usahihi.

 Kwa mujibu wa Dkt. Ngailo, taasisi hiyo inatarajia kuwa imepokea wanafunzi 7,000 ifikapo Jumamosi, huku mafunzo rasmi yakitarajiwa kuanza Jumatatu, Oktoba 26, 2026.

 Kwa upande wake, Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa DIT, Bw. Nicolous Busungu, amewahimiza wanafunzi wapya kuzingatia mafunzo ya utambulisho na maelekezo wanayopewa, akieleza kuwa ni muhimu kwao kufahamu katiba ya wanafunzi, kanuni na sheria za taasisi ili waweze kuzifuata katika maisha yao ya chuoni.

Amesema uelewa wa taratibu hizo utawasaidia wanafunzi kutekeleza majukumu yao ipasavyo, kuepuka ukiukwaji wa kanuni na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kitaaluma na kijamii.

Naye mwanafunzi mpya, Bi. Salma Ally, amesema kuwa yuko tayari kufuata maelekezo yanayotolewa na taasisi hiyo, akieleza kuwa mafunzo hayo yatakuwa na mchango muhimu katika safari yake ya masomo.

Vilevile, Bi. Eliminata Wakunda amesema mafunzo ya utambulisho yamewasaidia kupata uelewa kuhusu mambo mbalimbali yanayohusu maisha ya chuoni, hali inayotarajiwa kuwasaidia kuishi vizuri katika mazingira ya taasisi hiyo na kukamilisha masomo yao kwa mafanikio.

Post a Comment

0 Comments