
NA OKULY JULIUS, OKULY BLOG, DODOMA
MTOTO mwenye changamoto ya usikivu anaweza kukaa darasani bila kuelewa kinachofundishwa, mwingine mwenye usonji anaweza kutengwa na jamii kwa kudhani hawezi kujifunza, huku mwenye changamoto ya viungo akiachwa nyumbani kwa sababu familia haijui kuwa anaweza kupata elimu kulingana na uwezo wake.
Hata hivyo, hali hiyo inaanza kubadilika katika Jiji la Dodoma kupitia Kituo cha Utambuzi na Upimaji wa Kubaini Mahitaji Maalumu ya Ujifunzaji kwa Watoto (ESRAC), kilichopo Shule ya Msingi Nkuhungu.

Kituo hicho, kilichoanzishwa mwaka 2022 kwa gharama ya Sh milioni 48.6, kinalenga kuwabaini watoto wenye mahitaji maalumu mapema, kufanya tathmini na kuwaunganisha na huduma za elimu na afya kulingana na mahitaji yao.
Kuanzishwa kwa ESRAC kunatokana na maelekezo na mwongozo wa Serikali wa kuhakikisha watoto wenye changamoto za ujifunzaji wanatambuliwa mapema na kupata huduma stahiki badala ya kuachwa bila elimu au kufichwa majumbani.
KITUO KINAFANYA NINI?

Afisa Elimu Maalumu wa Jiji la Dodoma, Issa Kambi, anasema ESRAC inahusika na utambuzi, upimaji na upangaji wa fursa stahiki kwa watoto wenye mahitaji maalumu, hususan katika eneo la elimu.
Anasema kituo hufanya kazi kila siku, huku Jumanne na Alhamisi zikitengwa kwa ajili ya kliniki ambapo wazazi huwaleta watoto kwa uchunguzi, pamoja na wanafunzi kutoka shule mbalimbali wanaohitaji tathmini au mapitio ya awali.
Kwa watoto wanaobainika kuwa na changamoto za kiafya, kituo hutoa rufaa kwenda hospitali na kushirikiana na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Hospitali ya Benjamin Mkapa na Hospitali ya Taifa ya Magonjwa ya Akili Mirembe.
Kwa watoto wenye changamoto za macho, baadhi yao huunganishwa na huduma katika Hospitali ya Benjamin Mkapa pamoja na ufadhili wa Light for the World.
Aidha, wataalamu kutoka Mirembe, wakiwemo speech therapists, occupational therapists, physiotherapists na madaktari wengine, hutoa kliniki kituoni hapo na huduma hizo hutolewa bila malipo.
WATOTO 1,756 WAMEPIMWA

Msimamizi wa Kituo cha Upimaji ESRAC Nkuhungu, Neema Mukama, anasema tangu kuanzishwa kwake mwaka 2022, jumla ya watoto 1,756 wamepimwa, wakiwemo wavulana 905 na wasichana 851.
Kwa mujibu wa Neema, takwimu hizo zinaonyesha ukubwa wa mahitaji ya huduma za utambuzi na upimaji wa watoto wenye mahitaji maalumu, huku kituo kikiendelea kuwafikia watoto walioko katika jamii.
Anasema kupitia upimaji huo, watoto wamekuwa wakibainishwa changamoto zao na kuunganishwa na huduma zinazolingana na mahitaji yao, ikiwemo elimu, matibabu na huduma nyingine za kitaalamu.
WANAANZA KATA KWA KATA
Kambi anasema wataalamu wa kituo hicho wamekuwa wakifanya ubainishaji wa watoto wenye mahitaji maalumu kata kwa kata, hatua inayolenga kuwafikia hata wale ambao hawajawahi kufikishwa kituoni.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Denis Gondwe, anaeleza kuwa jiji hilo lina kata 41 na mitaa 222, ambapo timu za wataalamu hushirikiana na watendaji wa kata na mitaa, wenyeviti pamoja na wadau wengine kuwafikia watoto waliopo kwenye jamii.
Lengo, anasema, ni kuwabaini watoto ambao huenda hawajafikishwa kituoni na kuwawezesha kupata upimaji pamoja na huduma wanazohitaji.
Kambi anasema idadi ya watoto waliobainika imeongezeka kutoka takribani 600 miaka minne iliyopita hadi zaidi ya 1,700, jambo analolihusisha na kuendelea kwa zoezi la ubainishaji na uhamasishaji wa jamii.
BAADHI YA WAZAZI BADO WANAFICHA WATOTO
Pamoja na uwepo wa kituo hicho, bado kuna changamoto ya uelewa miongoni mwa baadhi ya wazazi na jamii, hali inayochangia baadhi ya watoto kuchelewa kupata huduma.
Neema anasema baadhi ya wazazi hawatoi taarifa sahihi kuhusu historia ya watoto wao wakati wa uchunguzi, jambo linaloweza kuwafanya wataalamu kutumia muda zaidi kubaini changamoto iliyopo.
“Katika zoezi la ubainishaji linalofanyika katika kata mbalimbali, tunakutana na maeneo ambayo ushirikiano na jamii unakuwa mdogo sana,” anasema.
Mwalimu Mkuu wa Kitengo cha Mahitaji Maalumu katika Shule ya Msingi Mlezi, Hashim Msemo, anasema changamoto nyingine ni baadhi ya watoto kufichwa majumbani na kufikishwa shuleni wakiwa wamechelewa.
“Mtoto unamkuta tayari ana miaka minane, tisa, wakati kwenye mwongozo wa upimaji inatakiwa kuanzia miaka mitano,” anasema.
WALIMU: MTOTO AKIBAINIKA, ANAPELEKWA KWENYE FURSA INAYOMFAA
Msemo anasema baada ya mtoto kubainika kuwa ana changamoto, wataalamu hushirikiana na wazazi, jamii, walimu na madaktari kutambua aina ya changamoto aliyonayo kabla ya kumpangia mazingira ya elimu yanayomfaa.
Anasema walimu nao wamepatiwa mafunzo ya namna ya kuwabaini watoto wenye mahitaji maalumu na kutumia mwongozo unaowaelekeza katika utambuzi na ubainishaji.
“Walimu pia tumepata mafunzo ya namna ya kuwabaini watoto wenye mahitaji maalumu na kutumia mwongozo unaotuelekeza kuhusu utambuzi na ubainishaji,” anasema.
Naye Mwalimu Digna Temba, anayefundisha wanafunzi wenye ulemavu wa macho, anasema walimu huangalia viashiria mbalimbali, ikiwemo changamoto za uoni, usonji na changamoto za ufahamu.
“Mtoto anapoonekana kuwa na changamoto, huwasiliana na wataalamu wa kituo cha Nkuhungu kwa ajili ya ubainishaji wa awali,” anasema.
SHULE YA MLEZI YAWAFIKIA WATOTO MITAANI

Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Mlezi, Magreth Kisanga, anasema shule hiyo yenye huduma za elimu jumuishi imekuwa ikiwafikia watoto wenye mahitaji maalumu kwa njia mbalimbali.
“Walimu hufanya home visiting kila Ijumaa kwa ajili ya kuwabaini watoto waliopo mitaani au wale ambao wameacha kuja shule kutokana na changamoto mbalimbali,” anasema.
Anaongeza kuwa mahusiano kati ya shule na jamii yamekuwa njia nyingine ya kuwafikisha watoto shuleni hapo.
Kwa mujibu wa Kisanga, Shule ya Msingi Mlezi ina wanafunzi 120 katika eneo la elimu maalumu, huku walimu wenye mafunzo maalumu wakiendelea kuwahudumia.
Hata hivyo, anasema changamoto ya usafiri ni miongoni mwa sababu zinazowafanya baadhi ya watoto kutohudhuria shule mara kwa mara.
WALIMU: WATOTO WANAWEZA KUBADILIKA
Msemo anasema baadhi ya watoto waliokuwa wamefichwa majumbani wameonyesha mabadiliko baada ya kuanza kupata elimu.
“Mfano, wapo watoto ambao walifika shuleni hapa wakiwa hawawezi kufanya baadhi ya shughuli za msingi, lakini baada ya kufundishwa wameanza kujitegemea zaidi,” anasema.
Anasema baadhi ya wazazi wamekuwa wakitoa ushuhuda wa mabadiliko yanayoonekana kwa watoto wao baada ya kuanza shule.
Hata hivyo, anasema changamoto ya usafiri bado inazuia baadhi ya watoto kuhudhuria masomo yao kwa mwendelezo mzuri.
DAKTARI: UCHUNGUZI WA MAPEMA NI MUHIMU
Daktari wa Kituo cha Afya Nkuhungu na mshiriki wa timu ya ubainishaji, Dkt. Rehema Magesa, anasema uchunguzi wa mapema unasaidia kubaini changamoto za mtoto kabla hazijawa kubwa zaidi.
“Watoto wenye changamoto za usikivu, uoni au changamoto nyingine za kiafya wanapaswa kubainishwa mapema na kupelekwa katika maeneo sahihi ya huduma,” anasema.
Dkt. Magesa anasema mojawapo ya changamoto wanazokutana nazo ni baadhi ya wazazi kutambua kwa kuchelewa hali za watoto wao, hasa kwa watoto wenye usonji.
Anaongeza kuwa imani potofu katika jamii nazo zinaweza kuchelewesha wazazi kutafuta ushauri wa kitaalamu.
Kwa mujibu wa daktari huyo, mtoto mwenye ulemavu anaweza kuwa na uwezo mkubwa katika eneo fulani hata kama anakabiliwa na changamoto katika baadhi ya masomo ya darasani.
CHUMBA MAALUMU CHA UPIMAJI WA USIKIVU
Katika kituo hicho pia kuna chumba maalumu kinachotumika kufanya ubainishaji wa awali kwa watoto wenye changamoto za usikivu.

Mwalimu Elizabeth Katunzi anasema kituo kina vifaa vya kisasa, vikiwemo audiometer na digital otoscope, vinavyosaidia kufanya uchunguzi wa awali wa masikio.
“Baadhi ya watoto wanaofikishwa hapa kituoni hugundulika kuwa na changamoto zinazoweza kutibiwa, kama nta nyingi au vitu vilivyoingia kwenye sikio na watoto hao hupewa rufaa kwenda hospitali kwa ajili ya matibabu,” anasema.
Anasema huduma ya uchunguzi wa awali kituoni hapo hutolewa bila malipo na baada ya mtoto kubainika kuwa na changamoto, hupangiwa shule kulingana na mahitaji yake.
WATOTO WAPELEKWA SHULE KULINGANA NA MAHITAJI
Kwa watoto wenye changamoto kubwa ya usikivu, wataalamu hutoa rufaa na baada ya kuthibitishwa na daktari hupangiwa shule zinazolingana na mahitaji yao.
Katunzi anasema baadhi yao hupelekwa Shule ya Msingi Dodoma Viziwi, wengine Hombolo na wengine katika shule jumuishi zilizo karibu na maeneo wanayoishi.
Lengo ni kuhakikisha mtoto hapotezi fursa ya elimu kutokana na aina ya changamoto aliyonayo.
WAZAZI: USAFIRI NI CHANGAMOTO
Kwa upande wa wazazi, changamoto kubwa iliyotajwa ni usafiri.
Farida Khamis, mzazi wa watoto mwenye mahitaji maalumu, anasema gharama za usafiri zimekuwa mzigo, hasa kwa familia zinazowapeleka watoto shuleni kutoka maeneo ya mbali.
“Nauli imekuwa ikifikia kati ya Sh3,000 hadi Sh5,000, hali inayotuwia vigumu sisi wazazi wenye kipato kidogo,” anasema.
Anaishauri Serikali kuangalia uwezekano wa kuweka usafiri maalumu au mabweni kwa watoto wenye mahitaji maalumu ili kupunguza mzigo kwa wazazi.
Licha ya changamoto hiyo, anasema anaridhishwa na huduma zinazotolewa kituoni, lakini anasisitiza umuhimu wa kutafutiwa majawabu changamoto ya usafiri kwa watoto wenye ulemavu.
“WATOTO HAWAPASWI KUFICHWA”
Wadau waliohojiwa wanatoa ujumbe unaofanana kwa jamii kwamba watoto wenye mahitaji maalumu hawapaswi kufichwa majumbani.
Msimamizi wa kituo hicho, Neema, anasema watoto wenye changamoto mbalimbali wanapaswa kufikishwa katika vituo vya upimaji ili kubaini fursa stahiki kulingana na uwezo wao.
Anasema hata mtoto mwenye usonji, changamoto ya usikivu, ulemavu wa viungo au changamoto ya ufahamu anaweza kupata elimu na kujifunza kulingana na uwezo wake.
Naye Dkt. Magesa anasisitiza kuwa watoto wenye ulemavu wana haki ya kupata elimu na huduma nyingine muhimu na wanapaswa kuonekana ili jamii iweze kuwasaidia.
SERIKALI YAOMBWA KUONGEZA VITUO NA MAFUNZO
Pamoja na mafanikio yaliyoelezwa, watendaji wa kituo wameainisha maeneo yanayohitaji maboresho, ikiwemo mafunzo ya mara kwa mara kwa wataalamu wanaotumia vifaa vya kisasa.
Mahitaji mengine ni kuongezwa kwa vituo katika halmashauri nyingine na kuimarishwa kwa bajeti ya shughuli za ubainishaji ili kuwafikia watoto wengi zaidi.
Neema anasema baadhi ya vifaa vya kidijitali vimepatikana, lakini mafunzo ya matumizi yake yanahitajika mara kwa mara ili kuongeza ufanisi wa huduma.
Anaongeza kuwa baadhi ya wazazi kutoka mikoa mingine, ikiwemo Manyara na Moshi, wamekuwa wakifika Dodoma kutafuta huduma za upimaji.
DODOMA YAENDELEA KUPANUA ELIMU JUMUISHI
Kwa mujibu wa Afisa Elimu Maalumu wa Jiji la Dodoma, Kambi, jiji hilo lina jumla ya shule 213, ambapo takribani shule 60 zimebainishwa kutoa huduma ya elimu jumuishi.
Aidha, takribani shule 11 zina vitengo vya watoto wenye mahitaji maalumu, huku halmashauri ikiendelea kutumia klabu za elimu jumuishi katika shule mbalimbali.
Kambi anasema klabu hizo ni sehemu ya kuwafundisha wanafunzi kuhusu elimu jumuishi na kuwasaidia kupeleka ujumbe huo katika jamii.
Takribani miaka minne tangu kuanzishwa kwa ESRAC Dodoma, kituo hicho kimekuwa sehemu ya utambuzi wa watoto wenye mahitaji maalumu na kuwaunganisha na huduma za elimu na afya.
Kupitia ubainishaji unaofanyika kituoni na katika jamii, watoto wanaobainika kuwa na changamoto wamekuwa wakipatiwa tathmini, huduma za awali, rufaa na kupangiwa mazingira ya elimu yanayolingana na mahitaji yao.
Hata hivyo, changamoto bado zipo, ikiwemo uelewa mdogo wa baadhi ya wazazi, watoto kufichwa majumbani, usafiri, upungufu wa walimu na wataalamu katika baadhi ya maeneo pamoja na mahitaji ya mafunzo na bajeti kwa ajili ya shughuli za ubainishaji.
Kwa wazazi na wataalamu, ujumbe wao ni mmoja: mtoto mwenye mahitaji maalumu hapaswi kubaki nyumbani kwa sababu ya changamoto aliyonayo. Anatakiwa kutambuliwa, kupimwa na kupewa fursa ya elimu inayolingana na uwezo na mahitaji yake.






0 Comments