Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Cde. Christopher Ngubiagai, amewataka wananchi wa wilaya hiyo kutunza mazingira kwa kusafisha fukwe, kuacha ukataji wa miti na kuhifadhi vivutio vya asili ili kuvutia watalii na kukuza uchumi wa eneo hilo.
Ngubiagai ametoa wito huo katika hafla ya uzinduzi wa Serengeti Safari Marathon – Ukerewe, akisisitiza kuwa hakuna utalii bila mazingira safi na mazuri yenye kuvutia wageni.
Akizungumza katika hafla hiyo, amesema wananchi wanapaswa kuanza kufundisha vijana umuhimu wa kutunza mazingira ili nao waweze kuendeleza utamaduni huo kwa watoto wao, kwa lengo la kuhakikisha mazingira yanahifadhiwa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
“Wafundisheni vijana wenu ili nao waje kuwafundisha watoto wao kutunza mazingira. Mazingira si mali ya Serikali pekee, bali ni yetu sote. Tuyatunze ili yavutie watalii na kukuza uchumi wetu,” amesema Ngubiagai.
Aidha, amewataka wafanyabiashara wa Ukerewe kuwa wakarimu kwa wageni, kuwapokea kwa upendo, kutoa huduma bora na kuuza bidhaa kwa bei za haki ili kuwavutia watalii na kuwafanya wafurahie huduma zinazotolewa wilayani humo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Serengeti Safari Marathon, Timoth Mdinka, amesema uzinduzi huo umefungua fursa za utalii Ukerewe, huku akieleza kuwa wanatarajia kupanda takribani miti 100,000 kwa lengo la kuhifadhi mazingira na kuboresha mandhari ya eneo hilo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, Vincent Mbua, amewapongeza watumishi wa umma walioshiriki katika mbio hizo na kuwataka kuwa mabalozi wazuri wa kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo Ukerewe, akieleza kuwa utalii ni mojawapo ya njia za kuongeza mapato ya halmashauri.
Akihitimisha hafla hiyo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ukerewe, Mhe. Ramadhani Mazige, amewapongeza wananchi waliojitokeza kuunga mkono na kushiriki katika mbio hizo, huku akiwataka vijana na wafanyabiashara kutumia fursa za utalii kujipatia kipato na kuchangia maendeleo ya wilaya hiyo.
Kaulimbiu: “Unlocking Blue-Green Tourism Economy in the Lake Victoria Basin” — Kufungua fursa za kiuchumi za buluu na kijani zinazotokana na vivutio vya utalii katika ukanda wa Ziwa Victoria.



















0 Comments